
Na Frank Shija, MAELEZO.Dar es Salaam
WANAFUNZI 3,918 wamechaguliwa
kujiunga na masomo ya kidato cha tano awamu ya pili kujaza nafasi
zilizokuwa wazi kutokana na ufinyu wa nafasi na baadhi ya wanafunzi
kutoripoti kwa wakati.
Taarifa iliyotolewa katika
vyombo vya habari na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Mussa
Ibrahim Iyombe ilisema kati ya wanafunzi hao wasichana ni 2,413 na
wavulana 1,505.
“Kuchaguliwa kwa wanafunzi hao
kumefuatia kuwapo kwa nafasi zilizoachwa wazi na wanafunzi ambao
hawajaripoti shuleni tangu kuchaguliwa kujiunga na kidato cha Tano
katika awamu ya kwanza” alisema Mhandisi Iyombe.
Aidha Mhandisi Iyombe
alibainisha kuwa kati ya wanafunzi 1,864 sawa na asilimia 47.58
wamechaguliwa kujiunga na masomo ya Sayansi na Hisabati ambapo kati yao
wasichana 1,099 na wavulana 765
Mhandisi Iyombe aliongeza kuwa
katika masomo ya Sanaa na Biashara wanafunzi takribani 2,054 (52.42%)
wamechaguliwa kujiunga na masomo hayo, ambapo kati yao wasichana ni
1,314 na wavulana 740.
“Wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2016 wanatakiwa kuripoti
katika shule walizopangwa kwa wakati. Endapo mwanafunzi atachelewa
kuripoti kwa zaidi ya siku 14 kuanzia tarehe ya tangazo hili atakuwa
amepoteza nafasi hii” alisema Mhandisi Iyombe.
Majina ya wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Tano awamu ya pili mwaka 2016
inapatikana kwenye tovuti ya Ofisi ya Rais -TAMISEMI ambayo ni www.tamisemi.go.tz.
No comments:
Post a Comment