Tuesday, 6 September 2016

Taarifa ya Jeshi la polisi Mkoani Mbeya kwa vyombo vya habari

POLISI
 Jeshi la Polisi mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu. Mafanikio yaliyopatikana katika Misako ni kama ifuatavyo:-
KUPATIKANA KWA SILAHA ZA KIVITA.
Mnamo tarehe 04.09.2016 majira ya saa 23:45 usiku huko katika kitongoji cha Sinza, Wilaya ya Chunya karibu na ofisi ya Usalama wa Taifa askari Polisi wakiwa Doria waliwatilia mashaka watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki isiyotambulika na kisha kuwafyatulia risasi na ndipo watu hao waliporusha mfuko ambao baada ya kupekuliwa uliokutwa na silaha moja aina ya Smg ambayo imefutwa namba zake, magazine mbili, bomu moja la kurusha kwa mkono na Risasi 24.
Watu hao wanaodhaniwa kuwa ni majambazi walikimbia na pikipiki na inadhaniwa kuwa mmoja kati yao amepigwa risasi. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa wananchi kwamba pale watakapoona mtu mwenye majeraha anayetibiwa bila kufuata utaratibu watoe taarifa.
KUPATIKANA NA NOTI BANDIA.
Katika msako uliofanyika mnamo tarehe 04.09.2016 majira ya saa 19:00 jioni huko Maeneo ya Mwanjelwa jijini, Mtu mmoja mkazi wa Nonde aliyefahamika kwa jina la JOSEPH SAUDEN (34) alikamatwa akiwa na noti bandia tatu za elfu tano zenye namba PP 1547999, GG 2937838 na BY 1547949 ambazo ni bandia zote zikiwa na thamani ya Tsh.15,000/=.
Mtuhumiwa alikamatwa akiwa anataka kununua nguo kwenye duka la Bwana NOVATUS KAVISHENI. Mtuhumiwa amekamatwa na upelelezi unaendelea.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Kumekuwa na matukio 01 ya mauaji kama ifuatavyo:-
MAUAJI.
  1. Mnamo tarehe 04.09.2016 majira ya saa 00:15 usiku huko katika kijiji cha Iduya Wilaya ya Mbarali, Mzee wa miaka 74 Mkazi wa Iduya aitwaye JACOB NGOLELA aliuawa kwa kukatwa shoka kichwani na shingoni.
Marehemu alikuwa na wake watatu na siku ya tukio alikuwa amelala nyumbani kwa mke mdogo aitwaye ELIZABETH KAMILO (62)   mkazi wa Iduya.
Mbinu iliyotumika na watu hao  ambao idadi yao haikufahamika  waliokuwa wamefunika nyuso zao kwa kofia za mizula  ni       kuondoa      matofali yaliyowekwa dirishani na kuingia ndani kisha kumkata     shoka           marehemu akiwa kitandani na kumuamuru mke wake asipige kelele.        Chanzo cha mauaji hayo ni mgogoro wa muda mrefu wa kugombea           mashamba   baina ya marehemu na mtoto wake aitwae MUSA JACOB        NGOLELA (42) mkazi wa Iduya ambaye amekamatwa. Upelelezi    unaendelea.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na matukio 02 ya ajali za vifo kama ifuatavyo:-
AJALI ZA VIFO.
  1. Mnamo tarehe 04.09.2016 majira ya saa 18:45 jioni huko katumba Wilaya ya Rungwe katika barabara kuu ya Tukuyu – Mbeya, Pikipiki isiyofahamika iliyotoroshwa baada ya ajali ikiendeshwa na AMANI LAWRENCE @ Mwangomwango (18) Dereva bodaboda, Mkazi wa Katumba iliacha njia na kupinduka na kusababisha kifo cha dereva huyo na majeruhi kwa AMED MWASAMBOMA (20) Mkazi wa Katumba ambaye alikuwa abiria wa pikipiki hiyo.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa hospitali ya Wilaya ya Rungwe na majeruhi amelazwa hospitalini hapo. Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa dereva huyo.
  1. Mnamo tarehe 04.09.2016 majira ya saa 12:15 mchana katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, iliyopo Jijini Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la AHABU KIMATILE (28) mkazi wa Mapogolo alifariki dunia wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.
Awali mnamo tarehe 03.09.2016 majira ya saa 14:05 mchana huko kijiji na kata ya Mapogolo, Wilaya ya Mbarali katika barabara ya Madibira kwenda Rujewa, marehemu akiendesha pikipiki  yenye namba za usajili T.416 BHT aina ya Sanlg iligongana na pikipiki nyingine yenye namba za usajili T.372 ABY aina ya Honda iliyokuwa ikiendeshwa na ZAKI YUSUPH (30) mkazi wa Rujewa na kusababisha majeruhi kwa waendesha Pikipiki hao na kulazwa hospitali ya Wilaya ya Mbarali kabla ya marehemu kuhamishiwa Rufaa Mbeya.
Chanzo cha ajali ni uzembe na mwendo kasi kwa waendesha pikipiki hao.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kutaka kupata mali au utajiri kwa njia ya mkato na badala yake wafanye kazi halali ili wapate kipato halali. Pia anasisitiza kuwa maendeleo hayapatikani kwa kufanya kazi hama biashara haramu, watumie fursa zilizopo Mkoa wa Mbeya kujitafutia ajira. Aidha anaendelea kutoa wito kwa madereva na watumiaji wa barabara kuwa makini hasa kwa kufuata na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoepukika.
Imesainiwa na:
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.

No comments:

Post a Comment