
Akiongea na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mhe. Nape amesema milango ipo wazi kwa wadau wengine wa michezo kujitolea katika kuiwezesha timu na hivyo kufanya vizuri katika mechi hii ambayo ni muhimu sana kushinda ili kufuzu kwa fainali hizo.
“Hii timu ni yetu sote hivyo inahitajika tuimiliki, tuepe nguvu, tuiombee ili iweze kufanya vizuri na hatimaye kufuzu kuingia fainali kwa kuitoa timu ya Congo-Brazzaville” alisema Mhe. Nape.
Waziri Nape amekutana na wachezaji wa timu hiyo ili kuwapa maneno ya faraja kabla ya kuanza kwa mechi na kuwataka watanzania kujitokeza kwa wingi uwanjani ili kuwapa motisha wachezaji kwa kuwashangilia na kuwatia moyo.
Mbali na hayo Waziri Nape alitoa ufafanuzi kuhusu matumizi ya kadi za kieletroniki zilizozinduliwa hivi karibuni kwa kueleza kuwa kadi hizo bado hazijaanza kutumika rasmi ila zitaanza kutumiwa katika mchezo baina ya Wabunge wa Simba na Yanga pamoja na Bongo Fleva.
Timu ya Serengeti Boys inaundwa na vijana wa Kitanzania wenye umri chini ya miaka 17 ambapo katika mchezo huo watahitaji ushindi na baadaye kufanya mechi ya marudiano mnamo Oktoba 2 mwaka huu nchini Congo-Brazzaville.

No comments:
Post a Comment