Sunday, 18 September 2016

Samatta kuendelea leo kusaka mabao

Baada ya kuanza vibaya hatua ya makundi ya Europa League kwa kufungwa 3-2 na Rapid Viena katika mchezo wa Kundi F wiki iliyopita, mshambuliaji wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta na timu yake ya KRC Genk leo wanarejea kwenye Ligi ya Ubelgiji.
Genk leo watakuwa wenyeji wa Anderlecht Uwanja wa Luminus Arena mjini Genk katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji, wakitoka kufungwa mechi mbili mfululizo, ukiwemo wa Jumapili iliyopita walipofungwa 2-0 na Standard Liege katika Ligi ya Ubelgiji pia.

Samatta amecheza mechi mbili mfululizo bila kufunga bao, kwani Alhamisi mabao yote mawili ya Genk yalifungwa na Leon Bailey, la kwanza dakika ya 29 na la pili dakika ya 90 kwa penalty.

Tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, Samatta amecheza jumla ya mechi 25 za mashindano yote, 18 msimu uliopita na saba msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.

No comments:

Post a Comment