Wednesday, 7 September 2016

Mkurugenzi wa Baraza la Mji Wete awataka wachuuzi wa samaki kutumia masoko yaliyopo

SAM_0984
Na Masanja Mabula –Pemba .
MKURUGENZI wa Baraza la Mji Wete  Philipo  Joseph amewataka wachuuzi wa samaki kuyatimia masoko yaliyopo kwa ajili ya biashara yao na kuacha kuuza samaki sehemu ambazo haziruhusiwi.
Amesema kuwa , Serikali imejenga masoko ili  wayatumie kwa ajili ya biashara ya samaki , na kwamba kuuza samaki sehemu zisozoruhusiwa kunachangia kunachangia uharibifu wa mazingira .
Akizungumza wakati wa operesheni ya kuwakamata wachuuzi wa samaki wanaouza samaki sehemu zisizoruhusiwa , Philipo amesema operesheni hiyo haina lengo la kumuonena mtu , bali imelenga kuimarisha usafi wa mji .
Aidha amesema kwamba , hakuna mchuuzi ambaye ataonewa na Baraza juu  , bali kila ambaye ataonekana kukiuka sheria na taratibu atawajibishwa ikiwa ni pamoja na kufikishwa mahakamani .
“Katika Operesheni hii hakuna mwananchi ambaye ataonewa na Baraza la Mji , lakini ambaye ataonekana kukiuka taratibu , lazima sheria zitachukua mkondo wake , na hili hakuna kuoneana muhali ” alisisitiza .
Akizungumzia kitendo cha dereva wa gari waliokuwa wamekubaliana kuwabeba wachuuzi kuwapeleka mahakamani , na kuwashusha njiani na kukimbia , alisema kwamba kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wanaendelea kumtafuta ili achukuliwe hatua za kisheria.
Nao wachuuzi wamuomba uongozi wa Baraza kuwaandalia mazingira ambayo yatawawezesha kuendesha biashara zao , wakati wakisubiri kukamilika ujenzi wa soko ili wahamie .
Mmoja wa wachuuzi hao Ali Abass alisema kwamba , ni budi Uongozi wa Baraza kuwapa muda wa kujitayarisha kuhamia katika soko kuu linaloendelea kujengwa , kwani masoko yaliyopo kwa sasa hayawatoshelezi.
“Soko la Bandarini lina vikuta si zaidi ya 50 wakati wachuuzi tuko zaidi ya 70 , hivyo tuamua wote kuingia itabidi samaki tupange chini ya sakafu jambo ambalo linahatarisha maisha ya wateja ”alieleza.
Operesheni hiyo iliyopewa jina la safisha Mji iliongozwa na Mkurugenzi wa Baraza hilo Philipo Joseph na itakuwa endelevu ambapo lengo ni kuhakikisha wachuuzi wanatii sheria bila ya kushrutishwa .

No comments:

Post a Comment