Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ametoa mwezi mmoja kwa Katibu Mkuu wa
Wizara anayeshughulikia Sekta ya Mawasiliano na Mtendaji Mkuu wa Kampuni
ya Simu nchini (TTCL), kuhakikisha kituo cha kutunzia taarifa (Data
Centre) kilichopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam kinaanza kufanya
kazi.
Prof. Mbarawa ametoa agizo hilo
kufuatia kukamilika kwa Data Centre hiyo miezi kadhaa iliyopita na
mahitaji ya wadau wa huduma ya kutunza kumbukumbu za taasisi zao katika
kituo hicho kuongezeka.
“Katibu Mkuu wa Sekta ya
Mawasiliano na Mtendaji mkuu wa TTCL hakikisheni kituo hiki
kilichojengwa kwa gharama kubwa kinaanza kutumika na kuwezesha mashirika
na taasisi mbalimbali kutunza kumbukumbu zao na kuiletea Serikali
mapato”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesema huduma ya
mtandao katika kituo cha Data Centre imeimarishwa kutokana na
kuunganishwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano hivyo itawarahisishia
wateja wake kuweka na kuchukua taarifa zao kwa haraka.
Akizungumza mara baada ya kukagua
maeneo mbalimbali unapopita Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano Prof.
Mbarawa amemtaka Mkurugenzi wa TTCL kanda ya Kaskazini Bw. Peter Lusama
kuhakikisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unapitishwa juu ya nyaya
katika maeneo yenye changamoto za mafuriko ili kuepuka uharibifu wa mara
kwa mara na usumbufu kwa watumiaji.
Aidha amezitaka taasisi za
Serikali na binafsi kukitumia kituo cha kisasa cha kuhifadhi taarifa
DATA CENTRE kutunza taarifa zao ili kuzihakikishia usalama na uhakika wa
kuzitumia wakati wote, ambapo asilimia 75 imetengwa kwa ajili ya
kutunza taarifa kutoka sekta binafsi na 25 itatunza taarifa za Serikali.
Kituo hicho ambacho ni cha kwanza
kujengwa katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ni fursa
mpya kwa wafanyabiashara na wadau mbalimbali wenye taarifa nyingi
kuzihifadhi na kuzitumia wanapozihitaji kinamilikiwa na Serikali na
ujenzi wake umegharimu takribani dola za kimarekani milioni 93.
Katika hatua nyingine Prof.
Mbarawa amekagua uwanja wa ndege wa Singida na mahali utakapojengwa
uwanja mpya na kusisitiza umuhimu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege nchini
kusimamia kikamilifu ujenzi wa uwanja wa ndege wa sasa ambao upembuzi
yakinifu wake umekamilika.
Amesema tayari Serikali
imebainisha viwanja 11 vya ndege nchini kote na kuvifanyia upembuzi
yakinifu kabla ya kuanza kuvijenga ili viweze kukidhi mahitaji ya soko.
Amevitaja viwanja hivyo kuwa ni
Lake Manyara, Musoma, Iringa, Tanga, Songea, Kilwa Masoko, Lindi,
Moshi, Njombe, Simiyu na Singida ambavyo vitapanuliwa na kujengwa kwa
kiwango cha lami.
No comments:
Post a Comment