Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka Watanzania, viongozi wa dini zote kushirikiana kwa pamoja kupiga vita matukio maovu ya mauaji yaliyotokea katika maeneo mbalimbali nchini.
Amesema anatarajia hali ya amani,
usalama na utulivu inaendelea kuwepo nchini, hivyo wananchi hawana budi
kushirikiana na kushikamana na Serikali katika kuhakikisha matendo
maovu hayatokei katika maeneo yao.
Waziri Mkuu ameyasema hayo jana
(Jumamosi, Juni 11, 2016) wakati alipowasili mkoani Geita kwa ajili ya
kuhudhuria ibada ya kuwekwa wakfu Padre Flavian Kassala kuwa Askofu mpya
wa Jimbo Katoliki Geita.
“Mfano tukio la Mwanza watu
wanavaa kanzu na wanaingia msikitini na kukuta wenzao wanafanya ibada
kisha wakawachinja, hii haiwezekani kwa binadamu wa kawaida hivyo
tushirikiane katika kupiga vita matendo haya,” alisisitiza.
Hivi karibuni jumla ya watu 15 waliuawa kwa kukatwakatwa na mapanga katika mikoa ya Mwanza,Tanga, Dar es Salaam na Mara.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa
Geita, Meja Jenerali Mstaafu, Ezekiel Kyunga amesema vitendo vya watu
kuuawa kwa kukatwa mapanga vimepungua baada ya kuanzisha kampeni maalumu
ya kukemea mauaji hayo.
Alisema katika kampeni hiyo
wameamua kuwatumia walimu, viongozi wa dini mbalimbali pamoja na wauguzi
ambao wamekuwa wakiwaelimisha wananchi kuachana na imani potofu za
kishirikina na badala yake wajikite katika masuala ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment