Serikali imesema itachukua hatua kali ikiwemo kumfukuza kazi na kumfikisha mahakamani mfanyakazi wa Mizani atakayebainika anajihusisha na vitendo vya kupokea rushwa ili kuruhusu magari kupita bila kupimwa uzito.w
Kauli hiyo imetolewa na Katibu
Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng.
Joseph Nyamhanga wakati alipokagua huduma za upimaji uzito wa Magari
katika Mzani wa Njuki Mkoani Singida.
Amesema hadi sasa kuna baadhi ya
wafanyakazi wa Mizani wameachishwa kazi kutokana na kujihusisha na
vitendo vya kupokea rushwa kutoka kwa madereva wa magari ya Mizigo na
abiria.
“Hatutasita kuchukua hatua kwa
mfanyakazi yeyote atakayejihusisha na vitendo vya rushwa, hatua kali
tutachukua dhidi yake ikiwemmo kumfikisha mahakamani”. Amesema Eng.
Nyamhanga.
Badala yake Eng. Nyamhanga
amewataka wafanyakazi wote wa Mizani nchini kufanya kazi kwa uadilifu
kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za uendeshaji wa Mizani ili
kuweza kuleta ufanisi katika vituo vya kazi.
Pia amewataka madereva wa magari
na abiria nchini kushirikiana na Wizara hiyo kwa kutoa taarifa za
Wafanyakazi wa Mizani wanaowaomba rushwa ili kuweza kuondoa kero hiyo
kwa wananchi wanaotumia hudum za Mizani nchini.
Vilelevile amewaasa madereva wa
magari ya mizigo kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari ili kuepusha
uharibifu wa barabara ambazo hujengwa kwa kutumia kodi za wananchi.
“Madereva mnawajibu wa kulinda
barabara hizi kwa kutozidisha uzito wa mizigo kwenye magari yenu ili
kuziwezesha barabara zetu zidumu kwa muda mrefu”. Amesisitiza Eng.
Nyamhanga.
Aidha, Eng. Nyamhanga amesema
Wafanyabiashara na madereva wa magari makubwa ya mizigo yaendayo nje ya
nchi kuchangamkia fursa ya kuwapo kwa stika maalum za magari hayo kwani
kutapunguza idadi ya vizuizi vya upimaji wa uzito na hivyo kuharakisha
safari zao.
Naye Msimizi wa Mzani wa Njuki
Mnanka Chile amewaomba madereva wa magari kuzingatia sheria na kanuni za
alama za barabarabi na kuwa makini pindi wanapokaribia seheme za Mizani
ya kupimia uzito wa Magari.
Katibu Mkuu Eng. Josph Nyamhanga
yupo katika ziara ya kukagua Miradi ya Ujenzi wa barabara kwa kiwango
cha lami, Vivuko na huduma za Mizani katika Mikoa ya Dodoma, Manyara
Singida na Mara.
No comments:
Post a Comment