Serikali
imeliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutoagiza
transfoma nje ya nchi na badala yake kutumia zinazotengenezwa hapa
nchini na kampuni ya Tanalec.
Agizo hilo
limetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe.
Dkt. Medard Kalemani alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru
Kusini, Mhe. Daimu Iddi Mpakate aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa
pesa kukamilisha miradi ya umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Dkt.
Kalemani alisema uzalishaji wa transforma ni mkubwa ikilinganishwa na
mahitaji ya bidhaa hizo kwa mwezi, hivyo hakuna sababu ya kuagiza
transforma hizo kwa bei kubwa wakati zinapatikana hapa nchini.
Kuhusu suala
la kugharamia nguzo kwa Mpango wa REA Dkt. Kalemani alisema mteja
hatakiwi kutozwa gharama yoyote ziadi ya Tshs. 27,000 fedha ya
kuunganishiwa umeme kwa mpango huu.
Dkt.
Kalemani alisema kuwa Serikali inatekeleza Mradi wa REA Awamu ya II
katika Wilaya ya Tunduru na kazi hii inategemewa kukamilika mwishoni mwa
mwezi Juni, 2016.
Alisema Kazi
ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia ya
umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa Kilomita 293. 2, na ujenzi wa
njia nyingine yenye msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita 76.1
na ufungaji wa transfoma 38 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa
awali 3,330
“Gharama ya
Mradi kwa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo Wilaya ya Tunduru ni Tsh. Bilioni
32.56,” alisema Dkt Kalemani na kuongeza kuwa mkandarasi amekwishalipwa
bilioni 27.22 sawa na asilimia 83.6 ya fedha.
Dkt.
Kalemani amesema kuwa katika Wilaya ya Tunduru ni vijiji vinne ambavyo
vimeunganishiwa miundombinu ya umeme na kufanyiwa majaribio kabla ya
kuwashiwa umeme.
Kwa mujibu
wa Dkt. Kalemani mkandarasi anaendelea kufunga transforma na Mita za
Luku katika vijiji 34 vilivyosalia kwa Wilaya ya Tunduru ili viweze
kupatiwa huduma ya umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
No comments:
Post a Comment