Thursday 31 March 2016

Vikundi vya Ujasiliamali Mkuranga Vyashauriwa kuwa katika Mwamvuli wa Vicoba ili Kupata Sifa ya Kukopeshwa

Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa, Bengi Issa mwenye kilemba, akizungumza kwenye kikao cha pamoja na Mbunge wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega kushoto kwake kwa ajili ya kuangalia namna ya kushirikiana naye kuwasaidia na kuwawezesha wananchi wa Mkuranga. Mbunge Mkuranga asaka uwezeshwaji wa wananchi wake

Na Mwamvita Mtanda,  
MBUNGE wa Jimbo la Mkuranga, wilayani Mkuranga, mkoani Pwani, Abdallah Ulega, jana amefanya kikao na Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Taifa (NEEC), Bengi Issa, kwa ajili ya kutafuta fursa ya kuwawezesha wananchi wilayani humo.
Mbunge wa Mkuranga, Mheshimiwa Abdallah Ulega, akizungumza jambo katika kikao cha pamoja na Mkurugenzi wa Baraza la Uwezeshaji la Taifa (NEEC), Bengi Issa, hayupo pichani.
Kikao hicho pia kilihusisha Mkurugenzi wa Uwezeshaji, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkuranga, ambapo Pamoja na mambo mengine, kilijadili namna ya kusaidia vikundi vilivyosajiliwa 285, vikundi vya vicoba 109, ufugaji wa nyuki, vikundi vya wanawake, vijana na waendesha bodaboda.
Akizungumza baada ya kikao hicho kumalizika, Ulega aliyewahi pia kuwa Mkuu wa wilaya Kilwa, Alisema kwamba lengo ni kuona wanananchi wa Mkuranga wanapiga hatua kutoka kwenye hali ya Ukata na kufikia kiwango kizuri, sanjari na kufanikisha maendeleo kwa wananchi wote.
Alisema kwamba kikao hicho kimemalizika kwa mafanikio ambapo ilishauriwa kuwa vikundi vya kukopeshana (VICOBA) inabidi viwekwe chini ya mwamvuli mmoja utakaoviwakilisha vyote.
“Hili litakapofanyika, Benki ya Posta Tanzania ina utaratibu wa kutoa mikopo ya riba ndogo kupitia Mwamvuli huo unaowakilisha vikundi vyote kwa pamoja, tukiamini kuwa itasaidia kwa kiasi kikubwa kufanikisha ndoto zetu.
“Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunaiweka Mkuranga katika kiwango kizuri ukizingatia kwamba Wilaya hii ipo karibu na jiji la Dar es Salaam, hivyo inaweza kukua kwa kasi kwa sababu mtu anaweza kuishi Mkuranga na akafanya kazi au kuingia na kutoka kwa urahisi wilayani kwetu,” alisema.
Aidha imeshauriwa pia kuanzisha SACCOS ya wafugaji wa nyuki ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo Ya vifaa kwa ajili ya ufugaji wa kisasa wa nyuki, ambapo wana vikundi wanatakiwa kuandaa mpango kazi wao utakaopelekwa Benki ya Maendeleo kwa ajili ya mkopo, ikiwa na lengo la kuhifadhi misitu na kuacha utafutaji wa kipato kwa njia ya kukata miti ili kuzalisha mkaa.

Barabara Ya Kigoma-Nyakanazi Kukamilika Mwezi Mei

1Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiwasili katika Kiwanja cha Ndege cha Kigoma tayari kuanza ziara ya ukaguzi wa miundombinu katika mikoa ya ukanda wa magharibi.
2Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) kuhusu ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na China Railway 50 Group.
3Ujenzi wa barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 inayojengwa na Kampuni ya  China Railway 50 Group ukiendelea.
4Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) akitoa maelekezo kwa wataalamu wa ujenzi wa kampuni ya China Railway 50 Group baada ya kukagua mitambo yao ya kupima na kutafiti udongo kabla ya kujenga barabara.
5Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa kofia) akitoa maelekezo kwa viongozi wa Wilaya ya Kasulu mara baaada ya kukamatwa kwa vijana wawili (waliokaa chini) kutokana na wizi wa nyaya za mkongo wa taifa, mkoani Kigoma.
6Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (aliyevaa koti la kaki) akiangalia athari za mmonyoko wa udongo zilizoathiri mkongo wa taifa wa mawasiliano katika eneo la Kidahwe mkoani Kigoma.
..
Makandarasi wanaojenga barabara ya Kidahwe-Kasulu Km 50 na Kibondo-Nyakanazi Km 50 wametakiwa kukamilisha ujenzi huo mwezi Mei mwakani badala ya Novemba ili kuharakisha mkakati wa Serikali wa kuufungua mkoa wa Kigoma kwa barabara za lami.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema hayo mara baada ya kukagua ujenzi wa barabara hiyo uliyogawanywa sehemu mbili, Kidahwe-Kasulu inayojengwa na China Railway 50 Group na Kibondo-Nyakanazi inayojengwa na Nyanza Road Works.
 
Prof. Mbarawa amewataka makandarasi hao kuongeza kasi ya ujenzi, vifaa na  wafanyakazi wenye sifa ili barabara hizo zikamilike kwa wakati na ubora unaotakiwa.
“Tutahakikisha ifikapo Juni mwaka huu tutakuwa tumelipa madeni yote mnayoidai Serikali hivyo fanyeni kazi kwa uhakika kwa kuwa katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Tano tayari tumeshawalipa makandarasi zaidi ya shilingi bilioni 725”, amesema Prof. Mbarawa.
Prof. Mbarawa amesisitiza kwamba nia ya Serikali ni kuifungua mikoa ya Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa kwa barabara za lami ili kufungua ukanda wa magharibi mwa nchi kibiashara kutokana na ukanda huo kuwa sehemu muhimu ya nchi katika uzalishaji na kiungo kikuu kwa nchi za Congo DRC, Burundi na Rwanda.

Katika hatua nyingine Waziri Prof. Mbarawa amewataka wafanyakazi wa Shirika la Reli (TRL), kulinda miundombinu ya reli na kujiepusha na vitendo vya hujuma ili kuliwezesha shirika hilo kupata shehena kubwa ya mzigo kufuatia wadau mbalimbali kuonesha nia ya kusafirisha mizigo kwa njia ya reli
“Serikali imewekeza vya kutosha katika Shirika la Reli hivyo mfanye kazi kibiashara ili mpate mzigo mkubwa wa kusafirisha”, amesisitiza Prof. Mbarawa
Akizungumza na viongozi wa mkoa wa Kigoma na taasisi zilizo chini ya wizara yake Prof. Mbarawa amewataka kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuzuia uvamizi na uhujumu wa miundombinu ya barabara, reli, na mkongo wa taifa wa mawasiliano na wote Watakaokiuka agizo hilo wachukuliwe hatua za haraka na za kisheria.

Prof. Mbarawa ametoa wiki moja kwa taasisi zilizo chini ya wizara yake kuhakiki wafanyakazi ili kubaini kama kuna wafanyakazi hewa.
Naye, Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), mkoa wa Kigoma, Eng. Narcis Choma amemhakikishia Waziri Prof. Mbarawa kuwa mkoa wa Kigoma Umejipanga vizuri katika kudhibiti uvamizi wa miundombinu ya barabara na wale Waliojenga ndani ya mita 22 kwenye barabara kuu wataondolewa maramoja bila kulipwa fidia.

Prof. Mbarawa yuko katika ziara ya kukagua miundombinu katika mikoa ya kanda ya Magharibi ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa Serikali wa uiboreshaji wa miundombinu Ya kanda hiyo ili kuiwezesha kufanya biashara kiurahisi na mikoa mingine ya Tanzania na nchi za Congo DRC, Rwanda na Burundi.

No comments:

Post a Comment