Wednesday 23 March 2016

TASAF Yatoa Milioni 137.8 kwa kaya Masikini 57 Serengeti

TASAFNa Chrispino Mpinge 

MPANGO wa Kunusuru Kaya Masikini Tanzania  (TASAF III) umetoa zaidi ya shilingi Milioni 137.8 kwa kaya masikini 3627 katika vijiji 57 wilayani Serengeti mkoani Mara.
Hayo yamesemwa na Mratibu wa TASAF Wilaya ya Serengeti Bi Nancy Nzota alipokuwa Akiongea na wananchi wa kijiji cha Gesarya, Kata ya Rung’abure  kuhusu malipo ya kaya hizo kuwa yamefikia awamu ya tano.

Alisema Malipo ya fedha hizo yameyotolewa katika kipindi cha utekelezaji wa mpango huo kwa mwezi Machi hadi Aprili 2016.

“Fedha hizi mnazopewa ni mbegu na mnapaswa kuzitumia kukidhi mahitaji muhimu yakiwemo ya Elimu, afya na kuanzisha shughuli za uzalishaji” alisema Bi Nancy.

Bi Nancy aliongeza kuwa, watendaji wa vijiji wanatakiwa kubaini kaya zinazotumia fedha hizo kinyume na matakwa ya mpango huo ambapo amewataka watendaji watakaogunduliwa Waondolewe katika uwakilishi wa kaya na mchakato wa kubadili wasimamizi/wawakilishi wapya Wa kaya zao ufanyike kwa utaratibu maalumu.

Aliwaonya Wanufaika wa mpango huo kutokutumia fedha hizo kwa shughuli zinazokinzana na Mpango huo kwani kufanya hivyo hakutawatoa wananchi katika hali ya umasikini.

Alisema kuwa elimu hasa ya ujasiriamali ilishatolewa kwa wanufaika katika kila kijiji juu ya kuanzisha shughuli za ufugaji, kilimo na biashara ndogo ndogo.

Aliongeza kuwa pia elimu hiyo huendelea kutolewa mara kwa kwa mara na wawezeshaji wa Mpango wa TASAF ambao hutoa elimu hiyo kwa wananchi katika kila awamu ya malipo.
Mpango huu ulizinduliwa mkoani Dodoma, Agosti 2012 na Rais mstaafu, Dk Jakaya Kikwete, Ambapo kwa Wilaya ya Serengeti malipo kwa kaya masikini lilianza rasmi Julai 2015 na limeonesha kuanza kuzinufaisha kaya hizo.

No comments:

Post a Comment