Mshambuliaji wa timu ya mpira wa
miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbaraka Yussuf Abeid (katikati)
‘anaposepa’ na kijiji yaani kuhama au kuondoka na idadi kubwa ya
watu/mabeki waliomzunguka wakiwamo Salum Mbonde, Shomari Kapombe na
Kiungo Aboubakar Salum katika mazoezi ya timu yanayofanyika Uwanja wa
mazoezi wa Kituo cha michezo cha Tolip (Tolip Sports City) hapa
Alexandria, Misri. Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti
kutoka Kampuni ya Bia ya SBL inajiandaa kucheza na Lesotho Juni 10, 2017
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania kucheza fainali za Kombe la
Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon. Picha
na Alfred Lucas wa TFF.
Mpaka leo asubuhi Juni 2, mwaka
huu, Kocha Mkuu wa timu ya mpira wa miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’,
Salum Mayanga pamoja na wenzake katika benchi la ufundi, wamekinoa
kikosi hicho kwa dakika 420 ndani ya Uwanja wa mazoezi wa Kituo cha
michezo cha Tolip yaani Tolip Sports City hapa Alexandria, Misri.
Kwa mujibu wa programu ya Kocha
Mayanga, Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia ya Serengeti kutoka Kampuni
ya Bia ya SBL itafanya mazoezi yasiyopungua dakika 1,500 katika kambi
iliyoanza Mei 31, 2017 usiku na kufikia kikomo Juni 7, mwaka.
Siku ya kwanza ya kambi Mei 31,
mwaka huu Kocha Mayanga alianza na dakika 120 za mwanzo baada ya
kusafiri salama kutoka Tanzania hadi hapa Misri.
Kila siku Taifa Stars ina programu
mbili ambako asubuhi timu inafundishwa kwa dakika 90 uwanjani kwa
mazoezi mbalimbali na kwa programu ya usiku ni dakika 120 ambako huanza
saa 3.00 (saa 2100) usiku na kumaliza saa 5.00 (saa 2300) usiku kwa saa
za hapa Misri.
Kwa msingi huo, Kocha Mayanga kwa
kusaidiana na benchi lake la ufiundi, anakionoa kikosi hicho kwa
takribani saa 25 kwa wiki, kabla ya kurejea nyumbani. Timu itarudi
Tanzania usiku wa kuamkia Juni 8, mwaka huu.
Ikiwa nyumbani Tanzania, Mayanga
atawanoa tena kwa dakika nyingine 180 tayari kabisa kuivaa Lesotho Juni
10, 2017 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mchezo huo umepangwa
kuanza saa 2.00 usiku.
Mchezo dhidi ya Lesotho ni muhimu
kwa Tanzania ikiwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’
kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika
(AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.
Mbali ya Lesotho na Tanzania,
mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia
wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza
pia kuwania nafasi hiyo.
Akizungumza mwenendo wa mazoezi
kwa saa 300 za mwanzo, Kocha Mayanga amesema: “Nafarajika vijana wangu
wameendelea kufunguka. Hapa hawana usumbufu wo wote, ni mazoezi na
kupumzika kulingana na ratiba na chakula.”
Mazoezi ya Mayanga hayathiri
maendeleo ya mwili wa binadamu kadhalika nguzo ya funga kwa wale ambao
wako kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani, kwani ratiba huonyesha
huanza kunolewa kuanzia saa 12.00 alfajiri – saa mbili baadaye baada ya
daku (Uhudumiwa daku kabla ya saa 11.00 alfajiri), lakini pia saa 3.00
usiku ikiwa ni saa mbili baada ya kufuturu (Futari ni saa 12.45 jioni).
Ikiwa hapa kambini, timu hupata
huduma zote kwa upande wa chakula na wachezaji wana faraja ya kizalendo
kuitumikia timu yao ambayo ina mtihani dhidi ya Lesotho wakijenga imani
kabisa kwamba watafanikiwa.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
No comments:
Post a Comment