Wednesday 28 June 2017

Serikali imeridhishwa na Utendaji kazi wa Mamalaka ya Maji Safi na Maji Taka


DW2
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo (katikati) akisisitiza jambo wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na DAWASA.Kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA  Romanus Mwangi’ngo na kushoto ni Meneja wa Kituo cha uzalishaji maji Ruvu Juu Bw. Emmanuel  Makusa. 
DW3
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo  akikagua miundo mbinu ya chanzo cha maji ruvu juu wakati wa ziara yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na DAWASA.
DW4
Meneja wa Kituo cha uzalishaji maji Ruvu Juu Bw. E. Mukasa  (katikati)akitoa maelezo kwa Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo.
DW5
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo akikagua moja ya mitambo katika chanzo cha maji ruvu juu,kulia ni Kaimu Mtendaji Mkuu wa DAWASA  Romanus Mwangi’ngo.
DW6
Sehemu ya miundo mbinu ya katika chanzo cha maji Ruvu juu.
DW7
Sehemu ya miundo mbinu ya katika chanzo cha maji Ruvu juu.
DW8
Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo akioneshwa ramani ya mradi huo na hatua iliyofikiwa katika ulazaji wa mabomba kutoka kwa meneja wa mradi huo unaoanzia katika chanzo cha mto wami,mradi unaotekelezwa na Kampuni ya WAPCOS ya India chini ya usimamizi wa DAWASA.
 (Picha na Frank Mvungi-Maelezo)

Frank Mvungi-Maelezo
Serikali imesema imeridhishwa na Utendaji kazi wa Mamalaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA)  katika kutekeleza miradi mikubwa ya maji kwa kuzingatia Sheria na Kanuni hali inayoongeza tija katika mamlaka hiyo.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na DAWASA  katika Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani  Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwagiliaji Prof. Kitila Mkumbo amesema moja ya miradi hiyo ni ule wa kupanua na kusambaza maji katika mji wa Chalinze utakaonufaisha wakazi zaidi ya laki mbili.
“Kwa ujumla naridhishwa na kazi inayofanywa na DAWASA  katika kutekeleza miradi  ya maji nawatia moyo muendelee kufanya kazi hii  kwa bidii ili azma ya Serikali kuwafikishia wananchi huduma ya maji kwa wakati itimie” Alisisitiza Prof. Mkumbo.
Akifafanua Prof. Mkumbo amesema  katika ziara yake amejionea na kukagua miundo mbinu ya kusambaza maji,ujenzi wa matanki ya kuhifadhi maji na miundo mbinu yote katika chanzo cha maji Wami kinachopanuliwa ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa Chalinze .
“Wananchi  wajenge utamaduni wa kutunza rasilimali zilizopo ikiwemo miundo mbinu ya maji mbayo inajengwa kwa gharama kubwa ili iweze kuwanufaisha Wananchi wote na kuchochea maendeleo” Alisisitiza Prof. Mkumbo
Mradi mwingine uliotembelewa ni ule wa uchimbaji visima vyenye urefu wa mita 600 kila kimoja vipatavyo 20 na kati ya hivyo 17 vimekamilika hivyo kuongeza upatikanaji wa maji ambao utachochea  maendeleo na ukuaji wa sekta ya Viwanda.
Visima hivyo vitawezesha kuzalishwa kwa lita milioni 260 za maji kwa siku zitakazotumika katika Wilaya ya Kigamboni  na Jiji la Dar es Salaam.
 
Kwa upande wake  Kaimu  Mtendaji  Mkuu wa DAWASA mhandisi Romanus Mwangi’ngo amesema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa vyanzo vya maji Ruvu Juu na Ruvu Chini na Visima vya Kimbiji na Mpera vitasaidia kufikisha kiwango cha maji yanayozalishwa kufikia lita milioni 756 zitakazosaidia katika kuondoa tatizo la maji katika Jiji la Dar es  Salaam.
 Aliongeza kuwa  kwa  upande wa mradi wa Chalinze vituo vya kusambaza maji takribani 236 vimeshajengwa kati ya 351 vilivyopangwa  hali inayoonyesha kuwa mradi huo unaendelea kutekelezwa kama ilivyopangwa na utakamilika mwezi oktoba 2017.
Ziara ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji na umwagiliaji kukagua miradi inayotelezwa na DAWASA katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani imehusisha vyanzo vya maji vya Ruvu Juu,Mradi wa uchimbaji  Visima virefu Kimbiji na Mpera,Chanzo cha maji Wami unakotekelezwa mradi mkubwa wa upanuzi na ulazaji mabomba, ujenzi wa vituo vya kusambazia maji na matanki ya kuhifadhi maji Chalinze.

No comments:

Post a Comment