Sunday 25 June 2017

Watumiaji wa Barabara Watahadharishwa Kuzingatia Sheria

muslimu
Frank Mvungi-Maelezo
Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limetoa tahadhari kwa watumiaji wote wa barabara nchini kuzingatia sheria ili kuepuka ajali hususani wakati wa sikukuu ya Eid el Fitri.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo Jijini Dar es Salaam na  Kaimu Kamanda Kikosi cha Usalama Barabarani Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Fortunatus Musilimu  uzoefu umeonyesha kuwa katika kipindi cha sikukuu madereva wamekuwa wakiendesha magari kwa mwendo kasi, kuyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kubeba abiria kupita kiasi hali inayoweza kusababisha ajali.
“Tutafanya operesheni kali barabarani, kuwapima madereva kiwango cha ulevi na watakaobainika wamelewa watakamatwa na kuwekwa mahabusu na kufikishwa mahakamani, nasisitiza kwamba,dereva anayetaka kuendesha gari asinywe pombe,akitaka kunywa pombe asiendeshe gari” alisisitiza Kamishna Musilimu katika taarifa hiyo.
Aidha taarifa imewatahadharisha wamiliki wa magari yatakayokodishwa kwenda maeneo ya Fukwe bila kibali kuwa yatakamtwa na wahusika kufikishwa mahakmani.
Pia alitoa wito kwa wazazi kuangalia usalama wa watoto wao na wasiwaache wakatembea peke yao barabarani bila uangalizi ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
Kwa upande wa madereva wa Pikipiki (Bodaboda) amesema kuwa nao wamekuwa wakipita taa nyekundu,wakiendesha pikipiki zao bila kuvaa kofia ngumu,kubeba abiria zaidi ya mmoja (mishikaki) na abiria hao kutovaa  kofia ngumu hivyo kuhatarisha Usalama wao.
 
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani limekuwa likihamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuzingatia sheria na matumizi sahihi ya barabara ili kuepuka ajali katika kipindi chote na hasa wakati huu wa sikukuu.

No comments:

Post a Comment