Thursday 22 June 2017

Multichoice Tanzania Yasaidia Watoto Yatima

unnamed
Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania Baraka Shelukindo akikabidhi mashuka kwa Mlezi wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Madinnah kilichopo Tandale jijini Dar es Salaam Kuruthum Juma (wa pili kulia). Wa pili Kushoto ni Malkia wa Taarabu Hadija Kopa na kulia ni  Muigizaji maarufu wa tamthilia ya Huba Riyama Ali ambao ni mabalozi maalum wa DStv. Hafla hiyo iliyofanyika mapema leo katika kituo hicho ambapo vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni mbili vikiwemo vyakula, mashuka, vyombo na mitungi ya kuzimia moto vilikabidhiwa
1
Watoto wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Almadinnah kilichopo Tandale wakipokea vyombo kutoka kwa Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania Baraka Shelukindo baada ya kupokea msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali kutoka kampuni hiyo jana.
2
Mshonaji katika mradi wa ushonaji wa kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Madinnah cha Tandale jijini Dar es Salaam Aziza Amri (wa pili kulia) akitoa maelezo kuhusu mradi huo unaofadhiliwa na kampuni ya Multichoice Tanzania. Kutoka kushoto ni Malkia wa mipasho Hadija Kopa ambaye ni balozi maalum wa DStv, BiKuruthum Juma ambaye ni mkuu wa kituo hicho, Baraka Shelukindo Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania na kulia ni Muigizaji maarufu wa tamthilia ya Huba Riyama Ali. Mbali na kutembelea mradi huo, Multichoice pia ilikabidhi vyakula na vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni mbili kwa kituo hicho

Kampuni ya Multichoice Tanzania imetoa zawadi ya sikukuu ya Idi kwa kituo cha kulelea watoto yatima cha Al-Madinnah kilichopo Tandale jijini Dar es Salaam. Msaada huo wa vyakula na vifaa mbalimbali umekabidhiwa kwa kituo hicho na Meneja Uendeshaji wa Multichoice Tanzania  Baraka Shelukindo katika hafla fupi iliyofanyika kituoni hapo ambayo pia ilihudhuriwa na mabalozi kadhaa wa DStv akiwemo malkia wa Taarab Khadija Kopa na muigizaji maarufu wa filamu na Tamhtilia ya HUBA ,  Riyama Alli.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Shelukindo amesema kwa takriban miaka mitano mfululizo Multichoice imekuwa ikikisaidia kituo hicho kwa mambo mbalimbali.  Amesema wanafanya hivyo kwa kutambua kuwa malezi ya watoto waishio katika mazingira magumu ni jukumu la kila mtu na kila taasisi. “Tunatambua kuwa jukumu la kuwalea watoto kama hawa ambao kwa sababu moja ama nyingine wamejikuta katika mazingira magumu ni letu sote. Hawa ni ndugu zetu, watoto wetu, na pia ni tegemeo kubwa kwa taifa letu, hivyo kuwasaidia ni jukumu letu”
Amesema mbali na kwamba Multichoice imekuwa ikikisaidia kituo hicho mara kwa mara kwa kuwapa vyakula na mahitaji mengine, lakini pia waliamua kufadhili uanzishwaji wa mradi wa ushonaji ambao unakisaidia kituo hicho katika kujiingizia kipato. “Tunajua kuwa chakula, malazi na mambo mengineyo ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya vijana wetu, lakini pia tuliona ni busara kuwawekea kamradi japo kadogo ambako wataweza kujipatia kipato. Tumefurahi sana kuona mradi huu unaendelea na tunaamini kuwa  wataweza kuuendeleza na kuukuza ili uwasaidia Zaidi.” Alisema Shelukindo.
Kwa upande wake Mkuu wa kituo hicho Mama Kuruthum Juma ameishukuru Multichoice Tanzania  kwa msaada wao wa mara kwa mara kwa miaka mingi sasa. Amesema kitendo cha Multichoice Tanzania kukisaidia kitua hicho kwa mambo mbalimbali hususan mradi wa ushonaji kumewasaidia sana katika kujipatia kipata japo kusaidia gharama za uendeshaji kituo hicho ambazo ni kubwa. “Kwa kweli gharama za uendeshaji kituo ni kubwa sana na kama mnavyofahamu watoto wanaolelewa hapa hawana uwezo na wengi wao hawana wazazi, hivyo ni jukumu letu kuwalea, kuwapa matibabu, na pia kuwasomesha, hili kwa kweli ni jukumu kubwa na tunahitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali” alisema Mama Kuruthum
Amesema idadi ya watoto imekuwa ikiongezeka lakini kituo hakina uwezo mkubwa kutokana na ufinyu wa eneo na bajeti hivyo akawaomba wadau wengine kuangalia uwezekano wa kukisaidia kituo hicho ili kiweze kuhudumia watoto wengi Zaidi.
Naye Malkia wa Taarabu – Khadija Kopa amesema amefarijika sana kuona Multichoice Tanzania inawajali watoto hususan wale waishio katika mazingira magumu ambao aghalabu husahaulika na jamii. “Kwakweli Multichoice Tanzania  wamefanya jambo la maana sana. Ni vyema tukaunganisha nguvu zetu kuwalea hawa watoto wetu kwani nao wana haki kama watoto wengine” alisema Kopa.
Naye muigizaji Riyama Ali amepongeza jitihada zinazofanywa na Multichoice Tanzania  pamoja na uongozi wa kituo cha Almadinna katika kuwasaidia watoto hao. “Watoto hawa ni hazina ya taifa. Tukiwasaidia hawa wakakua vizuri, wakapata elimu nzuri, kesho na keshokutwa tutapata wabunge humu, mawaziri, wakurugenzi, wanamichezo, wasanii na kadhalika. Tushirikiane kuwalea na hili ni jukumu letu sote na ni kitu kinacholeta Baraka” alisema Riyama.
 
Kituo cha Al-Madinnah Orphanage Centre kilianzishwa mwaka 2004 na kwa hivi sasa kituo hicho kinahudumia jumla ya watoto 65 ambapo 40 kati yao ni wavulana na 25 wasichana na wengi wao ni wanafunzi wa shule za msingi.

No comments:

Post a Comment