Monday 24 April 2017

Mvulana wa miaka 12 aendesha gari 1,300km Australia

Babarabara inayopitia Broken Hill, Australia
Mvulana wa umri wa miaka 12 alikamatwa na polisi baada ya kupatikana akiwa ameendesha gari umbali wa kilomita 1,300.
Mvulana huyo alisimamishwa na polisi waliokuwa wanashika doria karibu na Broken Hill jimbo la New South Wales baada ya polisi kuona bamba la gari lake likiwa linaning'inia.
Polisi wanasema mvulana huyo alikuwa anajaribu kuendesha gari lake umbali wa 4,000km kutoka Kendall jimbo la NSW hadi Perth, Australia Magharibi.
Alikamatwa na kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Broken Hill.
Wazazi wake, ambao walikuwa wamepiga ripoti kwa polisi kwamba mvulana wao alikuwa ametoweka, walifika na kumchukua Jumapili.
Kutoka Kendall hadi Broken Hill, mvulana huyo alilazimika kupitia mamia ya kilomita ya barabara laini, ambayo katika baadhi ya maeneo hupitia mashambani.
Vyombo vya habari vinasema huenda alifanikiwa kupitia maeneo hayo bila watu kumshuku kwa sababu kwa sura anaonekana kuwa na umri mkubwa kuliko umri wake halisi.
Meneja wa kituo kimoja cha mafuta katika mji wa Cobar jimbo la NSW alisema kwa sura anaonekana kuwa "wa miaka 19 au 20".
Polisi pia walisema kwamba licha ya umri wake kuwa miaka 12, kimo chake ni "karibu futi sita".
"Alikuwa amechukua gari la familia yake," naibu inspekta wa polisi Kim Fehon aliambia shirika la habari la Australian Associated Press.
"Wazazi wake walipiga taarifa kwamba alikuwa ametoweka, kwa hivyo walikuwa wanamtafuta."

Msemaji wa polisi katika jimbo la New South Wales walisema huenda akafunguliwa mashtaka chini ya Sheria za Watoto Wahalifu.

No comments:

Post a Comment