Tuesday, 11 April 2017

Mvua yatibua Ligi ya Kikapu RBA

. Mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimegeuka chungu kwa Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (RBA) baada ya mechi kadhaa kuahirishwa kutokana na Uwanja wa Ndani wa Taifa kuvuja maji.
Mechi nne kati ya tano zilizokuwa zichezwe juzi kwenye Uwanja wa Ndani wa Taifa zilishindikana kufanyika kutokana uwanja huo kuvuja na kujaa maji.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BD), Haleluya Kavalambi aliliambia gazeti hili kuwa wanapata wakati mgumu kuendesha ligi hiyo kutokana na uwanja kuwa mbovu.
“Uwanja umekuwa kikwazo kwetu kwani imebidi tuahirishe baadhi ya mechi kwa sababu ya mvua. Maji yanaingia ndani, sasa wachezaji hawawezi kucheza kwa hali hii.
“Tumekuwa tukiuomba kutumia Uwanja wa Don Bosco Upanga na huwa tunatumia mara moja moja kwa sababu wenyewe wanautumia. Uwanja wa Ndani ndiyo unatumika kwa mechi nyingi, lakini hali ya mvua imekuwa tatizo kubwa,” alisema Kavalambi.
Aliongeza, “Hivi sasa kuna mtu tunaongea naye aweze  kutudhamini na kutupa mabati ili tuzibe juu ya paa la uwanja kukabiliana na mvua.
Pia, tuna mpango wa kutafuta mafundi wa maturubai ili atupe bei tujue tunafanyaje na ligi iendelee bila tatizo,” alisema.
Pia, Kavalambi alisema wana mpango wa kuikumbusha Serikali kuhusu mpango wao wa kujenga uwanja mwingine wa Ndani wa Taifa utakaotumika kwa michezo mbalimbali. “Tunajua huu Uwanja wa Ndani sasa hivi ni kama gofu maana umechakaa sana na tunautumia kwa sababu hakuna uwanja mwingine, lakini tunakumbuka kulikuwa na mpango wa Serikali wa kujenga uwanja mwingine wa ndani kwa ajili ya michezo mingine  baada ya ule wa mpira wa miguu kukamilika.



“Hivyo tunataka tukutane na Waziri wa Michezo na baadhi ya viongozi ili kuwakumbusha mpango huo wa Serikali wa kutujengea uwanja kwani kama unavyoona hivi sasa tunapata shida mvua zikinyesha,” alisema Kavalambi.
Wakati huohuo, ligi hiyo itaendelea kesho kwa Pazi kuikabili JKT wakati Ukonga Kings itaumana na Chui.

No comments:

Post a Comment