Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na watoto kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya
kiserikali itahadhimisha siku ya Kimataifa ya Mtoto wa kike ili
kutekeleza Azimio la Umoja wa Mataifa lililopitishwa mwezi Desemba mwaka
2011 likizitaka nchi wanachama kuadhimisha siku hii kupinga ndoa za
utotoni.
Maadhimio haya yatafanyika
kitaifa katika Mkoa wa Shinyanga kuanzia tarehe 5 Oktoba, 2016 na kilele
chake kitakuwa tarehe 11/10/2016. Maadhimisho haya ni moja kati ya
jitihada za Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kuelimisha na
kuhamasisha jamii kutambua umuhimu wa kutetea haki za mtoto wa kike na
kufanya tathimini ya changamoto mbalimbali zinazomkabili mtoto wa kike.
Aidha Umoja wa Mataifa umetenga
siku hii kwa lengo la kutafakari uzingatiaji wa haki na ustawi wa mtoto
wa kike; na hivyo kuweka mipango thabiti ya kuboresha maisha yao na
kuwawezesha kupata haki ya kulindwa, kuendelezwa, kuishi, kushirikishwa
na kutobaguliwa katika familia na jamii zao.
Wizara ya Afya, Maendeleleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inatoa wito kushirikisha wananchi na
wadau wengine katika kuadhimisha siku hii, ili kupata ufahamu wa athari
za ndoa za utotoni, na kuzingatia kuwarithisha wasichana maadili mema na
maarifa ili kuwa na taifa lenye raia wema walioandaliwa kudumisha
uzalendo, amani, uadilifu, uaminifu, kujiamini, na kutoa mchango katika
maendeleo ya Taifa.
Kila mwaka, Maadhimisho haya huwa
yanabeba Kauli Mbiu yenye ujumbe mahsusi. Kwa mwaka 2016 Kaulimbiu
inasema “Mimba na Ndoa za Utotoni Zinaepukika Chukua Hatua Kumlinda
Mtoto wa Kike’. Kaulimbiu hii inahimiza wazazi, walezi na jamii
kutafakari na kuwekeza zaidi katika elimu ya mtoto wa kike ili
kuwajengea uwezo wa kuwa na mchango katika familia na taifa kwa ujumla.
Aidha mgeni rasmi katika
Maadhimisho haya ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
watoto, Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.).
No comments:
Post a Comment