Kiungo wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa, ametupa dongo kiaina kwa
wachezaji wa Ligi Kuu Bara akiwemo Laudit Mavugo na Method Mwanjale wa
Simba, baada ya kutua kwenye klabu yake mpya ya Fanja inayoshiriki Ligi
Kuu ya Oman.
Dongo hilo haliishii kwa wachezaji pekee, bali hata kwa timu za hapa
nyumbani zenye tabia za kufanya usajili wa wachezaji bila ya kuwapima
kama wapo fiti kila idara.
Ngassa amejiunga na timu hiyo hivi karibuni baada ya kuvunja mkataba na
Free State ya Afrika Kusini ambapo Fanja imempa mkataba wa miaka miwili
sambamba na straika, Danny Lyanga aliyekuwa Simba.
Kiungo huyo mshambuliaji siku chache baada ya kujiunga na timu hiyo,
ametupia picha kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa Instagram
ikionyesha vipimo alivyofanyiwa huku akiandika: “Na Bongo wapimwe kabla
ya kusajiliwa.”
Kwa mujibu wa picha hiyo, inaonyesha vipimo vyake alifanyiwa Septemba
21, mwaka huu kwenye Hospitali ya Badr Al Samaa chini ya daktari, Meena
Paul, yupo fiti na hana tatizo lolote.
Ikumbukwe kuwa, utaratibu huo wa kuwapima wachezaji kabla ya kusajiliwa
umekuwa mgumu kwa hapa nyumbani kwani mara kadhaa wachezaji wanasajiliwa
kimagumashi na mwisho wa siku wanakuja kugundulika wana matatizo ya
afya.

No comments:
Post a Comment