Beki wa kimataifa wa Yanga, Mtogo, Vincent Bossou, ameweka bayana kwamba
kwa sasa haoni straika wa kumsumbua wala anayemtisha kukutana naye
baada ya kumzima kirahisi mshambuliaji wa Simba, Mrundi, Laudit Mavugo
ambaye alisema kwamba angeisumbua ngome yao.

Mtogo huyo ambaye anaunda ukuta imara wa kikosi hicho akishirikiana na
Andrew Vicent ‘Dante’, mpaka sasa wameweka rekodi ya kuwa timu
iliyoruhusu mabao machache zaidi (mawili tu) kuliko timu nyingine,
ingawa inafungana na Kagera Sugar.
Bossou alisema kwamba licha ya washambuliaji wengi kuongea sana kuwa
watawapita na kuifunga timu hiyo, lakini wanashindwa kuonyesha uimara
wao pale wanapokutana nao.
“Kwa sasa hapa Bongo sijaona mshambuliaji ambaye anaweza kunitisha wala
kunifanya nimuwaze kukutana naye kwa sababu wote nawaona wa kawaida na
wengi wao wanaongea na tunapokutana nao wanakuwa na viwango vya kawaida
tofauti na wanavyoongea.
“Angalia hata katika mchezo uliopita yule Mavugo wa Simba, alitamba
kwamba atatufunga lakini cha ajabu tulimdhibiti kirahisi tofauti na
tulivyofikiria kwamba tungepata ushindani kutoka kwake na kila mtu
aliona jinsi ambavyo tulifanikiwa kazi yetu.
“Labda atokee straika wa nje ndiyo anaweza kutusumbua lakini siyo hawa wa ndani ambao wengi wako kawaida sana,” alisema Bossou.
No comments:
Post a Comment