Ibada ya hijja imemalizika rasmi
katika mji wa Makkah na Madina na mahujaji wa dini ya kiislamu zaidi ya
milioni 2 kutoka nchi zipatazo 164 wameanza kurejea makwao walikotoka.
Ibada ya mwaka huu imekuwa ya
mafanikio kwa kumalizika salama, hii ni kutokana na Serikali ya Saudi
Arabia kuwa na mipango madhubuti kwa kuimarisha miundombinu, usafiri,
ulinzi na usalama na kurekebisha dosari zilizojitokeza mwaka jana.
Maeneo ya misikiti yote miwili ya
Makkah na Madina yaliimarishwa na yanaendelea kujengwa ikiwa ni pamoja
na kupanuliwa ili kuongeza nafasi za kutosha kufanyia ibada.
Mahujaji kutoka Tanzania wapatao
2,000 wako salama na wao ni miongoni mwa walioshiriki katika ibada na
sasa wako njiani kurejea Tanzania. Hatua zilizochukuliwa na mamlaka za
ulinzi za Saudi Arabia ni pamoja na kuhakikisha kuwa makundi ya misafara
ya mahujaji hayagongani kati ya wanaokwenda na wanaorudi, njia
mbalimbali zilikuwa zikifungwa na kufunguliwa ili kuruhusu misafara
kwenda uelekeo mmoja bila kukutana. Hatua hii ilisaidia kuepusha ajali
kama iliyotokea wakati wa ibada ya hijja ya mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment