Lilian Lundo – MAELEZO
Zaidi ya wafanyabiashara 100
kutoka Tanzania na Kongo wanatarajia kushiriki kongamano la biashara
litakalofanyika Lubumbashi Kongo Septemba 22 mwaka huu.
Lengo la Kongamano hilo ni
kuimarisha uhusiano wa kibiashara, kuongeza kiasi cha mauzo ya nje na
kuboreshwa mazingira mazuri ya biashara kati ya nchi hizo mbili.
“Wafanyabiashara wa Tanzania wana
nafasi kubwa ya kupata soko nchini Kongo, kutokana na nchi hiyo
kutegemea bidhaa nyingi kutoka Tanzania kama vile samaki wabichi na
wakavu kutokana na nchi hiyo kutokuwa na bahari,” alifafanua Afisa
biashara wa TANTRADE Bi. Getrude Ngwesheni.
Aliendelea kwa kusema kuwa Kongo
wanaongea lugha ya kiswahili kuwasiliana, lugha ambayo inatumika na
watanzania wengi, hivyo itarahisisha mawasiliano katika shughuli za
biashara.
Kwa upande wake, Mratibu wa
Kongamano hilo kutoka Chama cha wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo
Tanzania (TCCIA) Bi. Anna Msonsa amesema kuwa kongamano hilo linatoa
fursa kwa wafanyabiashara wote kuanzia wa chini mpaka wale wakubwa na
kuwataka wafanyabiashara kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo.
Akitoa maelezo ya namna ya
kushiriki Kongamano hilo Afisa Miradi kutoka Kampuni ya 361 Bi. Naomi
Godwin amesema kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kujaza fomu ambazo
zinapatika katika ofisi za 361 digrii zilizoko Msasani pamoja na ofisi
za TCCIA na TANTRADE au kwa kutembelea tovuti ya www.tanzaniadrc.com.
Aidha, kongamano hilo limeandaliwa
na Ubalozi wa Tanzania Kongo, Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania
(TANTRADE), Chama cha wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania
(TCCIA), Shirikisho la wafanyabiashara wa Kongo (FEC), Chama cha
Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Taasisi ya Sekta Binafsi Nchi
Tanzania (TPSF), Kampuni ya 361 Degrees na mdhamini mkuu ambaye ni
Taasisi ya GSM Foundation.
No comments:
Post a Comment