Klabu ya Simba italazimika kulipa takriban Sh. milioni 396.82 kutokana na uharibifu walioufanya katika Uwanja wa Taifa wakati wa mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, imefahamika.
Aidha, tayari klabu hiyo imetozwa faini ya Sh. milioni tano kufuatia vurugu walizofanya Jumamosi katika mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamati ya Saa 72 ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) iliyoketi juzi – Simba pia imetakiwa kulipa gharama zote za uharibifu waliofanya.
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imesema zaidi ya viti 1781 vilivunjwa Jumamosi katika mchezo huo ulioingiza Sh. milioni 350 na kila kiti thamani yake ikiwa ni Sh. 220,000.
Kwa mantiki hiyo, gharama ya viti tu itakuwa Sh. milioni 391. 82, ambazo ukijumlisha na Sh. milioni tano za vurugu, zitaifanya Simba kulipa jumla ya Sh. milioni 396.82.
Lakini habari njema kwa Simba ni kwamba Nahodha wake, Jonas Gerald Mkude amefutiwa kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo huo, baada ya kubainika hakuwa na makosa.
Kamati hiyo pia imesema inawachunguza marefa wa mchezo huo, Martin Saanya, Ferdiand Chacha na Samuel Mpenzu kufuatia kuwapo tuhuma za uchezeshaji wa upendeleo.
Mashabiki wa Simba walifanya vurugu Uwanja wa Taifa Jumamosi baada ya Yanga kupata bao la kuongoza lililofungwa na mshambuliaji Mrundi Amissi Tambwe katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Tambwe alifunga bao hilo dakika ya 26, akimalizia pasi ndefu ya beki Mbuyu Twite na kugeuka mbele ya beki wa Simba, Novat Lufunga, kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Vincent Angban.
Bao hilo lilizua kizaazaa, wachezaji wa Simba wakimvaa refa Martin Saanya wakidai mfungaji, Tambwe aliushika mpira kabla ya kufunga. Na katika vurugu hizo, Saanya alimtoa kwa kadi nyekundu Mkude dakika ya 29 kwa sababu ndiye aliyekuwa mstari wa mbele. Simba ilisawazisha dakika ya 87 kwa bao la Shizza Kichuya.
Katika hatua nyingine, klabu ya Azam FC imetozwa faini ya Sh. 3,000,000 kwa kosa la kuvaa nembo ya mdhamini (Vodacom) upande mmoja badala ya pande zote mbili
No comments:
Post a Comment