Meneja masoko wa Benki ya CRDB
Fredrick Siwale akizungumza kwenye kilele cha wiki ya huduma kwa wateja
mjini Babati Mkoani Manyara, katikati ni Mkurugenzi wa mji huo
Fortunatus Fwema na Meneja wa CRDB Tawi la Babati Ronald Paul.
Meneja wa utawala wa Benki ya
CRDB Tawi la Babati Mkoani Manyara, Domitila Bugomola, akizungumza
kwenye kilele cha wiki ya huduma kwa wateja.
……………………………………………………………….
Benki ya CRDB Tawi la Babati
Mkoani Manyara, imefanikiwa kutoa mikopo ya sh16.1 bilioni kwa
wajasiriamali, watumishi wa Serikali, watumishi wa sekta binafsi, vyama
vya kuweka na kukopa na asasi za fedha.
Watumishi wa serikali na wasekta
binafsi 1,604 walikopeshwa sh12.8 bilioni na wajasiriamali 84 walikopa
sh3.3 bilioni ikiwa ni pamoja na wafanyabiashara na wakulima.
Meneja wa benki ya CRDB Tawi la
Babati, Ronald Paul akizungumza kwenye kilele cha wiki ya huduma kwa
wateja, alisema wamedhamiria kuwapa wateja wao huduma bora na
kuwanyanyua kiuchumi.
Paul alisema kwa muda wa miaka
miwili tangu waanzishe huduma ya benki hiyo mkoani Manyara, wamefanikiwa
kufungua matawi mengine madogo wilaya za Mbulu, Hanang, Simanjiro na
Kiteto.
Alisema pia wamefanikiwa kufungua
huduma za matawi madogo yaliyopo Magugu, Haydom na Mirerani ambayo
kupitia hayo wameweza kupata akaunti za halmashauri za wilaya.
Alisema kwenye matawi yao madogo
wamefanikiwa kuwa na huduma za ATM ambazo wamefungua 10 kwenye mkoa huo
na zinafanya kazi kwa muda wa saa 24.
“Kwa kipindi hiki tumefanikiwa
kuongeza ajira kwa watanzania hususani kwa wana Manyara kutoka
wafanyakazi 12 hadi 37 kutokana na matawi mengine madogo yaliyofunguliwa
katika wilaya mbalimbali,” alisema.
Alisema wamefanikiwa kupata amana
za sh11 bilioni zilizotokana na wateja 12,000 waliofungua akaunti za
akiba, watoto jumbo, akaunti za malkia, akaunti maalum, bidhaa nyingi za
kibenki za Simbanking, ATM na fahari huduma.
Mkurugenzi wa mji wa Babati
Fortunatus Fwema alitoa wito kwa benki hiyo kuwatafutia wateja wa mbaazi
wa nje ya nchi kwani hivi sasa wakulima wengi wanapata changamoto ya
soko la zao hilo.
Fwema alisema kutokana na benki
hiyo kutoa huduma za fedha hadi nje ya nchi hasa nchini India,
wangetumia fursa hiyo kwa kuwaunganisha wakulima hao moja kwa moja na
soko la mbaazi ambalo wanunuzi wengi hutoka nchini India.
No comments:
Post a Comment