Saturday, 10 September 2016

Yanga, Azam kuchuana kileleni

Dar es Salaam. Mchakamchaka Ligi Kuu Bara unaendelea wakati Yanga ikiwakaribisha vibonde Majimaji Uwanja wa Uhuru, huku vinara wa ligi hiyo Azam wataonyeshana ubabe Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Mbeya.
Mabingwa watetezi, Yanga wataingia uwanjani wakiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu na Ndanda, matokeo yaliyowanyima kusogea kileleni, hivyo wanahitaji ushindi mbele ya mashabiki wake watakaofurika kwenye Uwanja wa Uhuru ‘Shamba la bibi’.
Ili Yanga ikwee kileleni inatakiwa kuifunga Majimaji kuanzia mabao matatu ili ifikishe pointi saba, lakini iombee Azam ipoteze mchezo wake dhidi ya Mbeya City.
Kama Yanga itashinda mabao mawili au zaidi na Azam ikashinda basi mabingwa hao watetezi watashika nafasi ya pili wakiwa na pointi saba, wakati Azam itakuwa na pointi 10, kabla ya mechi ya kesho ya Simba dhidi ya Mtibwa Sugar.
Kocha wa Yanga, Hans Pluijm alisema wamejipanga kushinda dhidi ya Majimaji ili kujiweka vizuri kwenye ligi.
“Hatukupata  matokeo mazuri katika mchezo uliopita dhidi ya Ndanda, jambo lililotuhuzinisha, lakini tunatakiwa kuuangalia mchezo dhidi ya Majimaji ili tushinde,” alisema Pluijm.
Katika mchezo dhidi ya Ndanda, Pluijm amemchezesha Amiss Tambwe kama kiungo mchezeshaji kutokana na kukosekana kwa viungo wake, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Said Juma Makapu na Pato Ngonyani.
Uhondo mwingine utakuwa kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya, wakati wenyeji Mbeya City iliyoonja utamu wa kuongoza ligi itakapowakaribisha Azam FC.
Kocha wa Azam FC, Mhispania, Zeben Hernandez alisema malengo yao ni kurejea na pointi sita kutoka Mbeya na tayari wamepata pointi tatu na sasa wanazitaka tatu dhidi ya Mbeya City.

“Utakuwa mchezo mgumu kwani tunacheza ugenini, lakini wapinzani wetu wana timu nzuri,” alisema Hernandez.

Kocha wa Mbeya City, Kinnah Phiri amesema aliisoma Azam wakati ikicheza na Prisons na kujua mapungufu yao na kuyafanyia kazi ili kupata ushindi.

Michezo mingine inayotarajiwa kuvuta hisia za wengi ni ule wa Mwadui dhidi ya Stand United kwenye Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga, JKT Ruvu itaonyesha kazi na ndugu zao, Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani.

Kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Ndanda itakuwa wenyeji wa Kagera Sugar na African Lyon itaikaribisha Mbao kwenye Uwanja wa Karume, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment