Monday 29 May 2017

Ummy Mwalimu:Hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola hapa nchini

  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema kufuatia kupatikana kwa taarifa ya ugonjwa wa Ebola huko DRC Congo hakuna mgonjwa yeyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola hapa nchini hadi wakati huu.
Akizungumza na vyombo vya habari leo, Mwalimu alisema nchi yetu inapakana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hata hivyo kuna uwezekano wa ugonjwa huo kuingia hapa nchini kutokana na mwingiliano  wa watu, hasa wasafiri wanaotoka na kuingia.
Alisema kutokana na hali hiyo wizara inaendelea kuchukua tahadhari ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini.
"Wananchi wanashauriwa kutokuwa na hofu, waendelee kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huu.  Aidha Wizara inaendelea kusisitiza kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa huu hapa nchini," alisema Ummy.


Vilevile alisema wizara inaendelea kushirikiana na sekta mbalimbali katika kuimarisha ufuatiliaji na kutekeleza mikakati ya kudhibiti ugonjwa huo ili usiingie hapa nchini.

No comments:

Post a Comment