Friday 15 December 2017

Upendo Peneza awashangaa wanaohama vyama na kuliingiza taifa hasara kubwa

 Image result for Upendo Peneza
Mbunge wa Viti Maalum wa Chadema, Upendo Peneza amesema hana sababu za kuhama chama hicho kikuu cha upinzani nchini huku akiwashangaa wanaochukua uamuzi huo.
Peneza amesema kuhama chama kunasababisha hasara kwa Taifa kwa kuingia katika uchaguzi wa marudio huku akipendekeza uchunguzi ufanyike kwa waliohama ili kubaini ukweli wa sababu wanazozitoa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Desemba 15, Peneza amesema hajafikiria kuhama chama lakini anasikitika watu walioaminiwa na wananchi wakajiuzulu kwa kutoa sababu zisizoeleweka.

“Nimehusishwa mimi kuhama chama changu, sina sababu za kuhama ila ninachotaka ni hawa wanaohama watueleze sababu za kutuingiza katika hasara ya kurudia uchaguzi,” amesema Peneza.

“Sioni sababu ya kwenda kuunga mkono halafu utuingize gharama, yaani furaha zako utuingize sisi gharama, hapana…watueleze sababu zao,” ameongeza

Amesema kuna haja ya kupitia Katiba au kuendeleza mchakato wa Katiba ili kuwazuia kugombea wale wanaojiondoa kwa sababu zisizoeleweka.

Peneza amesema “kama unasema unaunga mkono, useme umewafanyia nini wananchi wako au kuunga mkono kwani lazima uchukue kadi ya chama kingine, Watanzania tunachezewa na watu na huu ni mchezo wa kisiasa unafanyika.”

Akizungumza kwa msisitizo, Peneza amesema “ninapinga haya kwa sababu pesa za wananchi hazitumiki vizuri, tunabana matumizi, tunapinga mafisadi halafu fedha badala ya kwenda katika maendeleo lakini tunakwenda katika uchaguzi.”

“Tusiharibu hela kwa kile wanachosema tunamuunga mkono, kama Rais atajenga daraja la Mwanza kwenda Sengerema, nitampongeza, kama chama changu kitanifukuza haya,” amesema Peneza

“Kiuhalisia shida bado kubwa, mbunge wa Siha angesimama akasema amenijengea shule, ametatua matatizo ya wakulima, ardhi sawa ila hayo hayajatekelezwa unamuungaje mkono.”

Kuhusu kuhusishwa kwake na kuhama, Peneza amesema wakati akigombea alijua kuna CCM yeye aliamua kuwa Chadema ingawa akadokeza kwamba hawezi kusema atakuwa Chadema maisha yote.


“Sisemi maisha yangu kwamba nitakuwa hapa, niliapa Novemba 2015 kuwa mbunge naomna Mungu anisaidie nimalize muda wangu salama na nitimize wajibu wangu niliopewa,” amesema Peneza.

No comments:

Post a Comment