Thursday 21 December 2017

Urafiki wawashukia wapangaji walioshindwa kulipa madeni yao


. Uongozi wa Kiwanda cha Urafiki umetangaza kiama kwa wapangaji zaidi ya 160 ukiwataka kulipa kodi la sivyo watawaondoa pasipo kuangalia hadhi ya mtu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Desemba 21,2017 naibu meneja wa kiwanda hicho, Shadrack Nsekela amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya wapangaji kushindwa kulipa madeni wanayodaiwa tangu mwaka 2015.
"Hakuna msalie mtume katika hili, tutawatoa wote bila kujali nani ni nani. Tumeanza kuwapa notisi tangu mwaka 2015 lakini hawalipi sasa tunawatoa," amesema Nsekela.
Amesema wapangaji waliopo katika kota za Urafiki jijini Dar es Salaam wanadaiwa kati ya Sh600 milioni na Sh1 bilioni.
Nsekela amesema wameanza kuwatoa wapangaji wa ofisi, huku wale wa makazi wakitakiwa kujiandaa wakati wowote nao watatolewa.
Akizungumzia suala hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya udalali ya Yono, Scholastika Kevela amesema baada ya siku 14 watapiga mnada mali walizokamata ili kufidia deni.

Amesema mbali ya ofisi, kuna yadi ya magari ambayo imefungwa na wahusika wakishindwa kulipa mnada utafanyika bila kumwonea haya mtu yoyote.

No comments:

Post a Comment