Friday 8 December 2017

Ronaldo atwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2017

Nyota wa   Real Madrid na timu ya Taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo amesema anataka kumalizia soka lake ndani ya Madrid baada ya usiku wa kuamkia leo, kutwaa tuzo ya  mchezaji bora wa dunia kwa mwaka 2017 (Ballon d'Or) ambayo hutolewa na (FFF).

Cristiano Ronaldo anashinda tuzo hiyo kwa mara ya tano na kuwa sawa na mpinzani wake wa karibu nyota wa Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina Lionel Messi ambaye ameshatwaa tuzo hiyo mara tano. “Nina furaha ndani ya Real Madrid na ninawashukuru wachezaji wenzangu kwa ushirikiano wanaonipa hadi kupata mafanikio haya, nina imani nitamaliza maisha yangu ya soka ndani ya Real Madrid”, amesema Ronaldo.
Kinyang'anyiro hicho cha kusaka tuzo hiyo kiliwahusisha wachezaji 30 waliong'aa kwenye soka duniani kwa mwaka 2017 ambao walitangazwa Oktoba 9 kabla ya mshindi ambaye ni Ronaldo kutangazwa usiku wa jana kwenye sherehe zilizofanyika jijini Paris Ufaransa.
Nyota wa Barcelona Lionel Messi ameshika nafasi ya pili, huku mchezaji nyota wa Paris Saint-Germain Neymar Jr akishika nafasi ya tatu. Nafasi ya nne imeshikiliwa na golikipa mkongwe wa Juventus Gianluigi Buffon. Nafasi ya tano imeenda kwa Luka Modric, sita ni Sergio Ramos na saba ni Klylian Mbappe.
Nafasi ya nane imeshikiliwa na kiungo wa klabu ya Chelsea N’Golo Kante, wakati mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski ameshika nafasi ya tisa na nafasi ya 10 ikifungwa na Harry Kane.

Msimu uliopita Ronaldo aliifungia Real Madrid mabao 42 yaliyoiwezesha kutwaa ubingwa wa UEFA kwa mara ya pili mfululizo na mara ya 12 katika historia ya klabu hiyo huku pia ikitwaa ubingwa wa La Liga kwa mara ya 33.

No comments:

Post a Comment