Na Kalonga Kasati
YANGA SC imeshinda 2-0 dhidi ya Sagrada Esparanca ya Angola katika mchezo wa kwanza wa mchujo kuwania kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika jioni ya leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Shukrani kwa wafungaji wa mabao hayo, Simon Happygod Msuva na Matheo Antony Simon, yote kipindi cha pili na sasa Yanga itahitaji sare katika mchezo wa marudiano wiki ijayo ili kuingia kwenye makundi.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na marefa kutoka Ghana, Joseph Odartei Lamptey aliyepuliza filimbi akisaidiwa na washika vibendera David Laryea na Malik Alidu Salifu, Yanga ilipoteza nafasi nyingi za kufunga
kipindi cha kwanza.kipindi cha pili pia kilianza kwa ugumu, Yanga wakiendelea kutengeneza nafasi nzuri na kushindwa kuzitumia, hali iliyoufanya mchezo uwe mgumu upande wao.
Kinara wa mabao katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Amissi Joselyn Tambwe ndiye ambaye hakuwa na bahati kabisa siku ya leo kutokana na kupoteza nafasi nyingi za wazi.
Baada ya kosakosa za muda mrefu, hatimaye vijana wadogo wazawa, Msuva na Matheo wakawainua mashabiki wa Yanga mfululizo kwa mabao safi.
Msuva alianza dakika ya 72 akimalizia krosi maridadi ya winga Godfrey Mwashiuya aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Malimi Busungu, kabla ya Metheo kufunga la pili dakika ya 90 kwa shuti la mbali.
Mshambuliaji Donald Ngoma ambao walikuwa wanatumikia adhabu za kadi za njano walizopewa mfululizo kwenye mechi dhidi ya Al Ahly mwezi uliopita.
Kikosi cha Yanga kilikuwa; Deo Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Oscar Joshua, Kevin Yondan, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Salum Telela/Mbuyu Twite dk46, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Malimi Busungu/Godfrey Mwashiuya Dk53, Amissi Tambwe na Deus Kaseke/Matheo Anthony dk77.
Sagrada Esperanca; Yuri JKose Tavazes, Roadro Juan da Semero/Paul Camufingo dk64, Dennis Conha Morais, Asenio Cabungula, Antonio da Silva Oliveira/Evanildo de Jesus Pedro dk64, Ntaku Zabakaka, Manuel Paulo Joao, Alentua Tangala Rolli, Osvaldochitumba Palana/Aderito Chosolla dk80, Manuel Sallo Conha na Antonio Kasule.
No comments:
Post a Comment