Mtu
mmoja mwanaume asiyefahamika jina, mwenye umri kati ya miaka 25 hadi 28
alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa
Mbeya.
Marehemu aliokotwa eneo la
Soweto, Kata ya Ruanda, Tarafa ya Iyunga tarehe 05.05.2016 majira ya saa
07:45 asubuhi akiwa uchi mahututi hajitambui na akiwa na majeraha
kichwani ya kupigwa na mtu/watu wasiofahamika.
Raia wema walitoa taarifa Polisi
na kufika eneo la tukio na kisha kumchukua mtu huyo hadi Hospitali ya
Rufaa Mbeya kwa matibabu na alifariki wakati akipatiwa matibabu.
Aidha chanzo cha mauaji hayo ni
kipigo na kiini cha tukio bado kinachunguzwa. Mwili wa marehemu
umehifadhiwa Hospitalini hapo. Upelelezi wa tukio hili unaendelea ikiwa
ni pamoja na kuwatafuta watu waliohusika na tukio hilo.
Katika Tukio la Pili:
Mtoto wa miaka mitatu
aliyefahamika kwa jina la ELIANA GOD mkazi wa Ilota Wilaya ya Mbeya
Vijijini alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na Gari lenye namba
za usajili T.119 ATY aina ya Toyota Dyana iliyokuwa ikiendeshwa na
dereva aitwaye HAULE KYENJE (54) mkazi wa Ilota.
Ajali hiyo ilitokea mnamo tarehe
05.05.2016 majira ya saa 13:00 mchana huko Kijiji cha Ilota, Kata ya
Mshewe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya.
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendo
kasi, mtuhumiwa amekamatwa. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali
Teule ya Ifisi. Upelelezi unaendelea.
Katika Tukio la Tatu:
Mtu mmoja mkazi wa Goye Wilaya ya
Mbeya Vijijini aliyefahamika kwa jina la DINALESS LUSWIGO (55)
alifariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na Gari iliyokuwa
ikiendeshwa na dereva asiyefahamika.
Ajali hiyo ilitokea mnamo tarehe
05.05.2016 majira ya saa 20:15 usiku huko Kijiji cha Goye, Kata ya
Ndanto, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya
katika barabara kuu ya Mbeya kwenda Tukuyu.
Chanzo cha ajali ni mwendo kasi,
mtuhumiwa alikimbia na gari mara baada ya tukio. Upelelezi unaendelea
pamoja na kumtafuta mtuhumiwa.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi JUSTUS A. KAMUGISHA anatoa wito
kwa madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na
kufuata na kuheshimu sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka
ajali zinazoweza kuepukika. Lakini pia anatoa wito kwa watumiaji wengine
wa barabara wakiwemo watembea kwa miguu nao wachukue tahadhari pindi
wanapotumia barabara.
Imesainiwa na:
(JUSTUS A. KAMUGISHA – SACP)
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.
No comments:
Post a Comment