Na Yahya NJenge
Taasisi ya kuzuia na Kupambana na
rushwa (TAKUKURU) yabaini kuwepo kwa sukari iliyofichwa tani 4,579.2
iliyonunuliwa toka Kiwanda cha Sukari Kilombero.
Kwa mujibu wa Taarifa iliyotolewa
leo jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU Valentine
Mlolowa Taasisi hiyo imeanza uchunguzi dhidi ya swala hilo kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa
mnamo tarehe 05 Mei, 2016 timu ya uchunguzi ilitembelea maghala yaliyopo
Tabata Jijini Dar es salaam na kubaini uwepo wa sukari hiyo.
TAKUKURU tayari imetembelea
Maghala ya mfanyabiasha Haruni Daudi Zacharia ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Al-Naeem yaliyoko Mbagala na Tabata ambaye ni miongoni mwa
wafanyabiashara wakubwa wa sukari hapa nchini na anayetuhumiwa kuficha
bidhaa hiyo. Ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha uchunguzi uliofanywa na
Taasisi hiyo ulibaini kuwepo kwa njama za dhati za kutouza sukari
iliyokutwa katika maghala hayo kulikofanywa na mfanyabiashara huyo kwani
hata Sehemu ya Maghala ilipo sukari hiyo hapakuwa na dalili za upakiaji
wa sukari hiyo ili iweze kusambazwa.
Taarifa hiyo imeendelea kufafanua
kuwa katika eneo la Kitumbini kumekuwa na wananchi wengi wanaohitaji
bidhaa hiyo na wachache sana waliweza kuuziwa licha ya ukweli kwamba
sukari ilikuwepo.
Katika uchunguzi wake TAKUKURU
pia imebaini kuwepo kwa mikakati ya dhati iliyokuwa ikifanywa na
mfanyabiasha huyo kwa kununua sukari yote toka viwanda vya ndani na
kisha kuihifadhi na kuuza bidhaa hiyo kidogo kidogo kwa wastani wa tani
250 kwa siku wakati alikuwa na uwezo wa kuuza zaidi jambo lililochangia
uhaba wa sukari katika soko.
Kuficha bidhaa ni kosa la uhujumu
uchumi na ni kinyume na Aya ya 3 Jedwali la kwanza Sheria ya Uhujumu
Uchumi Sura ya 200 [Chapisho la Mwaka 2002]. Serikali haitavumilia Hujuma za namna hii na itachukua hatua kali dhidi ya mfanyabiashara
yeyote ataekwenda kinyume na sheria hii.
TAKUKURU imetoa wito kwa
wafanyabiashara wote wa sukari kuacha vitendo vya kuficha Sukari na
vyombo vya uchunguzi vinafuatilia kote nchini na yeyote atakayebainika
kufanya hujuma hizo atakabiliwa na mkondo wa Sheria.
No comments:
Post a Comment