Wednesday, 18 January 2017

Taarifa ya Wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto


Coat_of_arms_of_Tanzania.svg
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inapenda kutoa taarifa kwa umma, kuhusu kuwepo kwa virusi vya mafua makali ya ndege katika nchi jirani ya Uganda.  Aidha taarifa hiyo imeeleza kuwa maeneo yalioathirika ni maeneo yanayozunguka ziwa Victoria pamoja na ziwa lenyewe. Ugonjwa huu umengundulika baada ya kuwepo kwa vifo vingi vya ndege pori katika maeneo  ya Lutembe beach, Masaka, Kachanga, Bukibanga na Bukakata ya nchini Uganda. Vilevile, vifo hivi vimetokea kwa baadhi ya ndege wafugwao (kuku na bata) na inahisiwa kuwa ndege hao wamepata virusi vya ugonjwa huo kutoka kwa ndege pori wanaohama kutoka nchi za Ulaya. Vifo hivyo vya ndege pori vilianza kuonekana tangu tarehe 2 Januari, 2017 na vimeonekana kuendelea hadi sasa. Kwa hapa nchini Tanzania hakuna vifo vya ndege vilivyoripotiwa hadi sasa.
Kwa kuwa hadi sasa hakuna binadamu yeyote aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo huko nchini Uganda, tahadhari inatolewa kwa kuwa  kuna uwezekano mkubwa wa ugonjwa kusambaa kwa binadamu ikiwa hatua madhubuti  za kujikinga hazitazingatiwa. 
UGONJWA WA MAFUA YA NDEGE 
Ugonjwa huu unasababishwa na virusi vya aina ya “Influenza” na huenezwa na ndege pori wanaohama hama (Migratory birds). Ndege hawa hubeba virusi vya ugonjwa huu bila ya kuonesha dalili za ugonjwa, hivyo huweza kuambukiza ndege wanaofugwa majumbani mfano kuku na bata wakati wanapokutana nao. Aidha ndege hao huweza kuambukiza ugonjwa huu kwa kupitia njia ya kinyesi ambacho hudondoshwa ardhini au kwenye mabwawa na madimbwi ya maji. 
Binadamu anaweza kuambukizwa ugonjwa huu kwa kugusana na ndege au kinyesi cha ndege aliyeathirika na ugonjwa huu. Hivyo ni muhimu kutokugusa mizoga ya ndege pori au kinyesi chake. Maambukizi ya ugonjwa huu yanaweza pia kutoka kwa ndege pori na kuathiri jamii ya kuku na bata na ndege ambao wanafugwa nyumbani. Hivyo wananchi wanaombwa pia kutoa taarifa iwapo wataona dalili zozote za ugonjwa na vifo katika jamii ya ndege hawa wa kufugwa pamoja na ndege pori.  Aidha, iwapo kutakuwa na maambukizi kwa jamii ya ndege hawa wa kufugwa, binadamu anaweza pia kupata maambukizi wakati wa kuchinja kuku, kunyonyoa manyoya, na wakati wa kutayarisha kabla ya kumpika. 
Vilevile kuna uwezekano wa virusi hivi  kuambukizwa kutoka kwa binadamu mwenye uambukizo kwenda kwa binadamu mwingine na hii ikitokea inaweza kusababisha mlipuko mkubwa unaoweza kusambaa pande zote za dunia (Influenza Pandemic). 
Maambukizi ya binadamu kwenda binadamu mwingine hutokea kwa njia ya kugusana na maji maji ya kutoka njia ya hewa iwapo mgonjwa atakohoa au kupiga chafya bila kufunika pua au mdomo, au kwa njia ya kugusa sehemu zenye virusi zilizochafuliwa na mgonjwa na mtu huyo kujigusa mdomomi au puani.
 
Dalili za ugonjwa wa mafua ya ndege ni pamoja na; homa kali, kutokwa na makamasi mepesi pamoja na mafua,  kuumwa na kichwa, kukohoa, vidonda kooni, kupumua kwa shida na vichomi. Vilevile baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa na dalili kama kuharisha, kutapika, kuumwa na tumbo na  kutokwa na damu puani na kwenye ufizi.
 
 
HATUA ZINAZOCHUKULIWA NA WIZARA KATIKA KUZUIA UGONJWA HUU USIINGIE NCHINI
Kuanzia mwaka 2007, nchi yetu imekuwa katika tahadhari ya ugonjwa wa mafua makali ya ndege na iliandaa Mpango Mkakati wa Kuzuia na kudhibiti ugonjwa wa mafua makali ya Ndege, ambao ndio ulitumika kuboresha utayari wa nchi na kuweza kufanikisha kudhibiti mafua makali ya nguruwe yaliyokuwa tishio duniani mwaka 2009. Aidha, mnamo mwaka 2012, Wizara kwa kushirikiana na Sekta za Mifugo, Maliasili na Taasisi za Utafiti za NIMR na TAWIRI, chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu iliweza kuandaa Mpango Mkakati wa miaka 5 wa Kudhibiti na Kuzuia magonjwa ya binadamu yanayoweza kutoka kwa wanyama, na mpango huu unatekelezwa hadi sasa. Kufuatia tishio la ugonjwa huu , mpango huu utatumika pia katika kutekeleza afua zilizoanishwa ili udhibiti  ugonjwa huu usiingie nchini. 
Vile vile  hatua zifuatazo zimechukuliwa baada ya kupata taarifa ya tahadhari ya ugonjwa huu hapo jana 16 Januari 2017; 
Kushirikiana na ofisi ya uratibu wa magonjwa yanayowapata binadamu na wanyama (Zoonotic Diseases) iliyoko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu (One Health Coordination Office), ambapo mkutano maalum umepangwa kufanyika tarehe 18 Januari 2017 ili kuweza kukutanisha wadau wote na hivyo kuandaa Mpango kazi wa namna ya kuzuia na kudhibiti ugonjwa huu.
Barua za tahadhari za ugonjwa huu zimepelekwa kwa Makatibu Tawala wa mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na . Fact Sheet (Ainisho Sanifu) za namna ugonjwa huu unavyoweza kuenezwa, kudhibitiwa pamoja na namna ya kutambua ugonjwa huu 
Kupitia kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya, Wizara imetoa maelekezo ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na utambuzi wa magonjwa (Surveillance) katika vituo vya kutolea huduma nchini kote. Aidha katika vituo maalum ambapo ufuatiliaji wa karibu umekuwa unafanyika kwa miaka kadhaa sasa, yaani katika mikoa ya Mwanza, Kigoma, Arusha, Manyara, Dodoma, Dar es salaam na Mtwara, tumeimarisha usimamizi wa ufuatiliaji wa karibu na kuelekeza kuwa kwa sasa wagonjwa wote wanoonekana kuwa na dalili zinazofanana na mafua makali ya influenza wachukuliwe sampuli ambazo zitapimwa kwenye maabara ya Taifa ya NHLQATC ambayo ina uwezo wa kufanya utambuzi huo.
Kuimarisha ufuatiliaji wa ugonjwa pia katika viwanja vya ndege, mipakani pamoja na bandari ili kubaini wagonjwa waingiao nchini wakiwa na dalili za ugonjwa huo.
Wizara pia inaandaa Timu kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo ili timu hii ya Taifa iweze kwenda kujenga uwezo wa kamati za kudhibiti milipuko ya mgonjwa na majanga hususani kwenye  mkoa wa Kagera na mkoa wa Mwanza. Aidha Timu hii pia itashirikiana na Timu za Mikoa kuandaa Mpango Mkakati wa Kudhibiti Ugonjwa huu usiingie ikiwa ni pamoja na kuainisha maeneo ya kuboresha ikiwemo upatikanaji wa vifaa kinga (Personal Protection Equipment, PPE)
Ili kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu jamii inaaswa kuzingatia yafuatayo:
Kutoa taarifa endapo wataona kutokea kwa  vifo vya ndege pori au wafugwao (kuku, bata na wengineo) kwa wataalamu wa mifugo, afya au ofisi ya serikali iliyo karibu nawe
Kutokugusa mizoga au ndege wagonjwa bila kutumia vifaa kinga
Kuepukana na tabia ya kuishi nyumba moja  na ndege wafugwao
Kuepuka kuchinja kuku au bata wanaoonyesha dalili yoyote ya ugonjwa 
Kunawa mikono vizuri kwa kutumia sabuni
Kupika nyama au mayai ya ndege kwa muda mrefu usiopungua nusu saa. .
Kuepuka kushika ndege wa porini na ndege wa majumbani wanaohisiwa kuwa na ugonjwa huu.
 
Hitimsho
Serikali inasisitiza kuwa mpaka sasa ugonjwa wa mafua ya ndege haujaingia hapa nchini ila upo katika nchi jirani ya Uganda katika jamii ya ndege pori kwa sasa. Kwa kuwa magonjwa hayaangalii mipaka, tunahitaji kuchukua tahadharii madhubuti ili kuzuia ugonjwa huu usiingie hapa nchini. Hivyo Wananchi wanahimizwa kuzingatia kanuni za afya za kuzuia ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa mara moja waonapo vifo vya ndege au kuku. Pia wanatakiwa kuripoti haraka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya mara waonapo dalili zozote za ugonjwa huu. Vile vile wananchi wanatakiwa kutokuwa na hofu kwani Serikali imejiandaa na itachukua hatua madhubuti za kudhibiti ugonjwa huu.
Mhe. Ummy Mwalimu (Mb)
Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na Watoto.
Tarehe 18 Januari, 2017

No comments:

Post a Comment