Na Is-haka Omar, Zanzibar.
Katibu wa Idara ya Kamati Maalum
ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu
amesema chama hicho kitaendelea kuishauri serikali na kutumia rasilimali
zake katika kusimamia sera na mikakati yake katika kuimarisha huduma
na fursa za kimaendeleo kwa wananchi.
Alisema malengo hayo yatafikiwa
endapo wafuasi wa Chama hicho na wananchi kwa ujumla watawaunga mkono,
kuwaamini na kuwachagua wagombea wanaopeperusha bendera ya CCM kwa kila
uchaguzi wa kisiasa ili waweze kuwaletea wananchi maendeleo kupitia
Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho.
Hayo aliyasema wakati akitoa
taarifa kwa Vyombo vya Habari juu ya maandalizi ya ufungaji wa Kampeni
za Chama hicho katika Uchaguzi mdogo wa jimbo la Dimani Unguja, alisema
maandalizi ya kufungwa kwa kampeni hizo yamekamilika kwa kufuata
miongozo, ratiba na masharti ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo alisema
Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dr. Ali Mohamed Shein anatarajiwa
kuwa mgeni rasmi katika ufungaji wa kampeni hizo zitakazofanyika
Januari 21 mwaka huu kuanzia majira ya saa 8:00 mchana katika Kiwanja
Cha Shule (Skuli) ya Fuoni Wilaya ya Magharibi “B” Unguja.
Alisema Dr. Shein ambaye pia ni
Rais wa Zanzibar atawahutubia wananchi kwa kueleza sera, mikakati na
muelekeo wa utekeleza wa shughuli za kimaendeleo zilizotekelezwa na
Chama hicho na zinazotarajiwa kutekelezwa katika maeneo mbali mbali
nchini hasa katika jimbo la Dimani.
Katibu huyo alisema viongozi
wengine watakaohudhuria Kampeni hizo na kupewa fursa ya kuzungumza na
wafuasi wa Chama hicho ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Abdulrahman Omar
Kinana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai pamoja na
viongozi na watendaji ngazi mbali mbali za taasisi hiyo.
Aidha alisema matarajio ya CCM
katika Uchaguzi wa Jimbo hilo ni kuendeleza ushindi wa kihistoria
kutokana na wananchi wa rika mbali mbali kumkubali mgombea wa Chama
hicho, Juma Ali Juma na kuahidi siku ya uchaguzi watamchagua rasmi bila
pingamizi awe Mbunge wa jimbo hilo.
“ Tunawaomba wafuasi wetu na
wananchi kwa ujumla mjitokeze kwa wingi katika Mkutano wa Ufungaji wa
kampeni za CCM kesho (leo) ili muweze kusikiliza sera na mipango
endelevu inayotekelezeka kwa vitendo itakayoelezwa kuwa ufasaha na Dr.
Shein pamoja na viongozi wengine.
Pia wale ambao ni wakaazi na
wapiga kura halali wa Jimbo la Dimani tuendelee kuhamasishana nyumba
kwa nyumba ili siku ya uchaguzi Januari 22 mwaka huu, tujitokeze kwa
wingi katika vituo vya kupigia kura kwa lengo la kumpa ridhaa Juma Ali
Juma aweze kuwatumikieni kupitia vipaumbele vyake.”, alieleza Waride na
kuongeza kuwa CCM ndio Chama pekee kinachotambua thamani na utu wa
makundi yote ya kijamii yaliyopo nchini.
Hata hivyo aliwasihi wafuasi wa
CCM kufuata utaratibu na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoashiria vurugu
na uvunjaji wa kanuni za wapiga kura siku ya uchaguzi badala yake wale
waliotimiza umri wa kupiga kura na wamekamilisha taratibu zote kisheria
wafike mapema katika vituo kwa kupiga kura na kurudi nyumba kusubiri
matokeo.
Uchaguzi huo unafanyika kufuatia
aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani Unguja, Hafidh Ali Twahir kufariki
Dunia ghafla mwaka uliopita akiwa katika utekelezaji wa Majukumu yake
huko bungeni Mjini Dodoma.
No comments:
Post a Comment