“Siku ya Ukoma Duniani”
huadhimishwa kila mwaka, Jumapili ya mwisho wa mwezi Januari. Mwaka huu
maadhimisho yanafanyika tarehe 29 Januari 2017. Siku hii iliasisiwa na
mwandishi wa habari mfaransa, Raoul Follereau aliyetumia muda wake
mwingi kuzunguka dunia kueleza hali duni ya maisha ya watu walioathirika
na ugonjwa wa ukoma.
Lengo kuu la kuadhimisha siku hii
ni kuukumbusha umma wa watanzania kuwa sote tunao wajibu wa kushiriki
kikamilifu katika vita ya kupambana na ugonjwa wa ukoma nchini. Siku hii
ni muhimu kwa jamii kukaa kitako na kutafakari madhara na shida
zinazotokana na maradhi ya ukoma. Tatizo kubwa la ugonjwa huu ni
kuvishambulia viungo vya mwili wa binadamu na kusababisha kukatika
viungo na hivyo kupelekea ulemavu wa kudumu ambao ndio hasa
huutambulisha ugonjwa huu kuliko hata dalili zake.
Maadhimisho ya Siku ya Ukoma
Duniani yanatupa fursa kama nchi kujitathmini na kuangalia harakati zetu
katika kuutokomeza kabisa ugonjwa wa ukoma katika Taifa letu. Kimsingi,
napenda kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuwa ukoma bado upo hapa
nchini kwetu na hivyo basi tuna wajibu wa kukabiliana nao. Takwimu
zinatuonyesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kutokomeza
ugonjwa huu kutoka kiwango cha utokomezaji cha watu 0.9 kati ya watu
10,000 mwaka 2006 na kufikia kiwango cha watu 0.4 kati ya watu 10,000
mwaka 2015. Kwa maana nyingine katika kila watanzania 10,000 kiwango
cha watu wenye ugonjwa wa ukoma sasa ni watu 0.4 mwaka 2015 kutoka
wastani wa wagonjwa 0.9 katika watu 10,000 mwaka 2015. Haya ni mafanikio
makubwa sana kwa sababu kiwango cha kimataifa cha utokomezaji ukoma
kinatakiwa kuwa chini ya mgonjwa 1 katika watu 10,000.
Japokuwa mwelekeo wetu kama nchi
unaonyesha tunapiga hatua nzuri, bado kuna wilaya na mikoa ambayo bado
tatizo la ukoma lipo juu na watu wengi wanazidi kuathirika. Mikoa na
wilaya ambazo bado zina wagonjwa wengi wa ukoma ni Lindi (Lindi
Manispaa, Liwale, Lindi na Ruangwa), Morogoro (Halmashauri ya Ulanga,
Kilombero na Mvomero), Dar es Salaam (Manispaa ya Temeke na Kigamboni),
Tanga ( Halmashauri za Muheza, Mkinga na Pangani), Mtwara (Halmashauri
ya Nanyumbu na Newala), Rukwa (Halmashauri ya Nkasi), Pwani (Halmashauri
ya Rufiji na Mkuranga), Geita (Halmashauri ya mji Geita na Halmashauri
ya Chato), Tabora (Halmashauri ya Sikonge), Mwanza (Halmashauri ya
Kwimba na Misungwi), na Ruvuma (Halmashauri ya Songea na Namtumbo).
Mikoa na halmashauri hizi haina budi kuongeza juhudi za ziada na
kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa ukoma kabla ya mwaka 2030 kama
yalivyo malengo ya maendeleo endelevu ya dunia. Endapo tutaongeza
jitihada katika maeneo haya, sina shaka kuwa nchi yetu itatokomeza
kabisa ugonjwa wa ukoma hata kabla ya mwaka 2030.
Ugonjwa wa ukoma unatibika na
kupona kabisa. Mgonjwa akijitokeza na kugunduliwa mapema hupona vizuri
bila madhara yoyote. Lakini, iwapo mgonjwa atachelewa kujitokeza na
kupata matibabu mapema, atakuwa katika hatari kubwa ya kupata madhara
ikiwa ni pamoja na ulemavu wa kudumu. Hivyo katika siku hii ya
maadhimisho ya siku ya Ukoma Duniani nitoe rai kwa watu wote wanaougua
ukoma nchini kwenda katika vituo vya tiba ili kupata huduma ya tiba.
Katika miaka 10 iliyopita,
ugonjwa wa ukoma peke yake umeongeza idadi ya watu wenye ulemavu wa
kudumu zaidi ya 2,800 hapa nchini na kwa mwaka 2015 tu, walemavu wapya
wapatao 300 waligunduliwa miongoni mwa wagonjwa wapya wa ukoma, kati ya
hao watoto walikuwa 26. Ulemavu unaotokana na ukoma unazuilika na hakuna
sababu ya kuendelea kuona idadi kubwa ya nguvu kazi yetu inakuwa
tegemezi na mzigo mkubwa kwa jamii yetu kwa sababu ya Ukoma.
Tunapoadhimisha Siku ya Ukoma duniani, napenda kutoa rai kwa jamii
kushiriki katika kuwabaini wagonjwa wa ugonjwa na kuwahimiza kwenda
kwenye vituo vya tiba ili kuepusha ulemavu wa kudumu hasa miongoni mwa
watoto.
Ugonjwa wa ukoma huchukua miaka
mingi, hadi mpaka miaka 30 kati ya maambukizi hadi ugonjwa unapojitokeza
na kuonyesha dalili. Hivyo tuonapo dalili za ugonjwa huu miongoni mwa
watoto ni dhahiri ya kuwa ni maambukizi ya hivi karibuni na kuwa
maambukizi bado yanaendelea katika jamii. Hali itakuwa mbaya zaidi kama
mtoto hatagunduliwa mapema kabla ya kupata madhara ya ulemavu. Kazi
kubwa iliyombele yetu sasa ni kuwaepusha watoto na ulemavu unaotokana na
ukoma. Katika muktadha huu, Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Tuepuke ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa watoto”.
Kauli mbiu hii inatutaka wagonjwa
wa ukoma hasa watoto wagunduliwe mapema kabla ya kupata ulemavu na hasa
pale zinapojitokeza dalili za mwanzo za ugonjwa huu. Hivyo basi, kila
mmoja wetu katika maeneo ya mijini au vijijini nchini Tanzania, tujenge
tabia ya kuwachunguza watoto wetu kama wana dalili za ugonjwa huu au
la. Na endapo tutabaini dalili za ugonjwa huu miongoni mwa watoto basi
tuhakikishe tunawapeleke katika vituo vya kutoa tiba maramoja ili
kuwezesha ugonjwa kugunduliwa mapema kabla ya mtoto kupata ulemavu na
hasa pale zinapojitokeza dalili za mwanzo za ugonjwa wa ukoma.
Ukoma huenezwa kwa njia ya hewa
toka kwa mtu anayeugua na ambaye hajaanza matibabu. Dalili za ukoma ni
pamoja na baka au mabaka yenye rangi ya shaba mwilini. Mabaka haya
hayaumi wala hayawashi bali hupoteza hisia unapoyagusa na yanaweza
kujitokeza mahala popote mwilini, kuanzia kichwani hadi miguuni. Napenda
kutoa wito kwa kila mtu na familia kujijengea tabia ya kujichunguza
kila wakati na pale utakapoona dalili hizo nenda kituo cha huduma za
afya kwa ajili ya uchunguzi, ushauri na tiba.
Matibabu ya ukoma yanatolewa bila
malipo yoyote katika vituo vyote vya huduma, vya serikali na pia vya
binafsi. Serikali itahakikisha zipo dawa za kutosha na zinazopatikana
kwa wakati wote na kwa kila mgonjwa wa ukoma mahali popote nchini.
Tutaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa umma na kwa watoa huduma
hususani katika maeneo ambayo bado ukoma ni tatizo kubwa.
Ningependa kutoa wito kwa
halmashauri zote ambazo bado hazijafikia viwango vya utokomezaji wa
ugonjwa wa ukoma kuweka katika mipango kazi yao huduma za uchunguzi wa
ukoma ngazi ya kaya na hasa kuwafanyia uchunguzi wa mara kwa mara watu
wanaoishi na wagonjwa wa ukoma.
Vile vile, naziagiza halmashauri
zote nchini kuhakikisha zinawabaini walemavu wote, hasa wale wenye
ulemavu unaotokana na ukoma na kuwaweka katika mpango wa matibabu ili
kuzuia madhara zaidi yanayoweza kujitokeza baada ya kumaliza matibabu na
kupona ukoma
Aidha naziagiza halmashauri zote
nchini kuendesha uchunguzi wa ugonjwa wa ukoma kila wanapoendesha
kampeni yoyote ya upimaji wa afya za wananchi katika maeneo yao.
Mathalani, wakifanya kampeni ya upimaji wa mabusha, kichocho, kisukari
au magonjwa mengineyo, wawapime pia na ukoma. Kwa njia hii, tutaweza
kuwafikia watu wengi zaidi na kuwaokoa kwa kuwagundua na kuwaponyesha
mapema na hivyo basi kulipunguza tatizo la ulemevu huu kama siyo
kulikomesha kabisa.
Mwisho napenda kuwashukuru wadau
wote ambao wamekuwa wakitusaidia katika kudhibiti ukoma nchini wakiwemo
Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Ukoma la Ujerumani (GLRA),
Shirika la Madawa la NORVATIS, na Mhe. Yohaei Sasakawa, balozi wa amani
wa Umoja wa Mataifa katika harakati za kutokomeza ugonjwa wa ukoma.
Pia natoa shukrani za pekee kwa
mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Mama Janeth Magufuli
kwa misaada ya hali na mali anayoitoa kwa walemavu walioathirika na
ukoma katika makazi ya wasiojiweza sehemu mbalimbali nchini. Vile vile,
natoa shukurani kwenu wanahabari kwa elimu mnayoitoa kwa wananchi kuhusu
masuala mbali mbali ya uboreshaji wa afya ya watanzania, nawaomba
muendelee na juhudi hizo na mshiriki pia kikamilifu kuuelimisha umma juu
ya ugonjwa wa ukoma. Tulipofikia siyo pabaya lakini bado tunahitaji
kuweka juhudi kubwa zaidi ili kuumaliza ukoma na athari zake zote katika
jamii na hasa ulemavu ambao kwa namna yoyote ile unazuilika.
Ukoma unatibika na mgonjwa kupona
kabisa. Tujitokeze mapema wakati tukibaini dalili za awali ili
tuchunguzwe, tutibiwe na kujiepusha kabisa na balaa la ulemavu usio wa
lazima.
“Tuepuke ulemavu unaotokana na ukoma miongoni mwa watoto”.
Asanteni kwa kunisikiliza.
27/01/2017
No comments:
Post a Comment