Tuesday 24 January 2017

Marekani yajitoa Ushirikiano wa biashara na Pasifiki

Donald Trump akiwa White House
Rais wa Marekani Donald Trump amefanya kile alichokiita siku yake ya kwanza kuanza kazi katika utawala wake, kutokana na uamuzi alioufanya wa nchi yake kujiondoa katika mpango wa Ushirikiano wa kiuchumi wa nchi zinazounganishwa na bahari ya Pasifiki.
Ameonya pia kuyapa adhabu makampuni ya nchi hiyo yanayopeleka kazi nje ya nchi.
Makubaliano ya Mpango wa Ushirikianio wa Kibiashara wa nchi zinazounganishwa na Bahari ya Pacific TPP, yalijadiliwa na utawala wa Rais Barack Obama.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Sean Spicer anasema hatua hiyo ni dalili ya kuanza kwa enzi mpya ya sera za biashara za Marekani.
''...Kama alivyokuwa akisema Rais mara nyingi, hii ni aina ya makubaliano ya mataifa mengi na si kwa maslahi mazuri kwetu, na amekua akienda haraka kuboresha sera za kibiashara ambazo zitaongeza ushindani wa wafanyakazi wa Marekani na uzalishaji...'' Alisema Sean Spicer
Amesema amri hiyo ya Rais inaongoza katika enzi mpya ya sera za biashara ya Marekani, ambayo utawala wa Trump utapata fursa ya kufanya biashara na washirika wake duniani kote.

Lakini si hatua hiyo tu aliyoichukua Rais Trump, katika wiki yake ya kwanza ofisini, Rais Trump pia amerejesha amri ya kupiga marufuku utoaji wa fedha za serikali kwa makundi ya kimataifa ambayo yanazitumia katika kushughulikia ama kujadili utoaji mimba kama njia moja wapo ya uzazi wa mpango.

Uamuzi huo ni taarifa ya kwanza ya utawala mpya wa Marekani kutoa kuhusiana na misaada inayotoa kimataifa.
Utawala unaongozwa na chama cha Republican nchini Marekani mara zote umekuwa ukipiga marufuku msaada wa serikali kwa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa ambayo yanatoa huduma za utoaji mimba.

Wakati huohuo Baraza la Senete nchini Marekani limemthibitisha Mike Pompeo kuwa mkurugenzi mpya wa Shirika la Ujasusi nchini humo CIA.
Waandishi wa habari wanasema kazi yake ya kwanza itakuwa kurejesha uhusiano mzuri katui ya shirika hilo na Rais Donald Trump, ambaye amekuwa akilikosoa kwa kile ilichosema kwamba Urusi ilimsaidia wakati wa uchaguzi

No comments:

Post a Comment