Saturday, 28 January 2017

Watanzania milioni 1.9 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa majisafi na salama

  Watanzania milioni 1.9 wanatarajiwa kunufaika na mradi wa majisafi na salama wenye thamani Dola 225 milioni za Marekani, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB).
Kati ya watu hao, 700,000 wanatoka Jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha uchumi wa Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na WB kwa vyombo vya habari jana, ilieleza kuwa hatua hiyo inafuatia Bodi ya benki hiyo kupitisha Januari 23.
Pia, ilieleza kuwa mpango huo mpya uliopitishwa na Muungano wa Maendeleo ya Kimataifa (Ida),  utasaidia kuimarisha uwezo wa mipango ya rasilimali za maji na usimamizi nchini.
“Katika Jiji la Dar es Salaam, watu wengi wakiwamo wanawake  hutumia muda mwingi kutafuta maji. Jambo hili linawaweka mbali na elimu na shughuli za uzalishaji, hivyo mradi utatatua changamoto hizi,” alinukuliwa Mkurugenzi Mkazi wa WB, Bella Bird anayesimamia nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia.
Bird alisema makadirio  ya ongezeko la watu yanaonyesha asilimia 54 ifikapo mwaka 2030, watakuwa wanaishi katika miji midogo na mikubwa kutoka asilimia 24.4 kwa mujibu wa Sensa ya Makazi na Watu mwaka 2012.

No comments:

Post a Comment