Friday 20 January 2017

Mloganzila Hospitali kupunguza wagonjwa

MLO4
    Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Sekta ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni sekta muhimu sana katika kujenga uchumi wa nchi kwani bila rasilimali watu wenye afya njema, nchi haiwezi kuwa na uchumi ulio imara.
Katika kuimarisha rasilimali watu itakayochochea maendeleo ya nchi, Serikali ya awamu ya tano kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inajitahidi kuhakikisha huduma za afya za uhakika zinatolewa kwa wingi katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa kutambua umuhimu wa suala hilo, Serikali ilianzisha ujenzi wa Hospitali ya kisasa katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi (MUHAS) kilichopo eneo la Mloganzila nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam ambayo tayari imekamilika na inatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa mwezi Januari mwaka 2017.
Ujenzi wa Hospitali hiyo ya kipekee na ya aina yake katika eneo la Afrika Mashariki na kati ulianza mnamo Aprili 24 mwaka 2104 na kukamilika Agosti 31 mwaka 2016 ambapo kwa sasa wataalamu wanaendelea kuweka vifaa tiba na kufunga mifumo ya vifaa vya tehama ili kurahisisha kazi hospitalini humo.
Hospitali hiyo ya kisasa ilijengwa kwa mkopo wa riba nafuu kutoka Serikali ya Korea Kusini pamoja na fedha ya Serikali ya Tanzania hivyo hadi kukamilika kwake imegharimu jumla ya dola za kimarekani milioni 94.5 ambazo ni sawa na Tsh.206.7 bilioni.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo hicho (Muhimbili), Eligius Lyamula amesema kuwa Serikali iliamua kutoa kiwanja chenye ukubwa wa hekari 3800 kwa ajili ya kupanua shughuli za Chuo na kuweza kuzalisha wataalam wa kada mbalimbali za afya ili kuweza kutatua changamoto za afya zinazowakabili wananchi.
“Hospitali hii ina uwezo wa kuweka vitanda 571 na inategemewa kutibu magonjwa makubwa hivyo tunategemea kupunguza idadi kubwa ya wagonjwa wanaotibiwa katika Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili pamoja na kupunguza gharama kwa wanaoenda kutibiwa nje ya nchi,” alisema Lyamula.
Aliongeza kuwa Hospitali hiyo inategemea kutoa huduma za kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wanaosomea sekta ya afya ili kuondokana na tatizo la upungufu wa watumishi wa kutosha katika sekta ya afya na wasio na ujuzi katika taaluma hiyo.
Lyamula alifafanua kuwa Serikali iliona tatizo la upungufu wa watumishi wa afya hivyo ikaamua kutafuta fedha kwa ajili ya kujenga chuo hicho ambacho kitakuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 15,000 kutoka wanafunzi 4000 wanaodahiliwa kwa sasa hivyo ni dhahiri kabisa kuwa wagonjwa watapata huduma za uhakika.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mh.Paul Makonda alipotembelea Chuo hicho mnamo Novemba 26 mwaka 2016 kwa ajili ya kuangalia maendeleo ya ujenzi wa chuo hicho alitoa ushauri kwa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuweka sheria kwa wanafunzi wanaosomea masomo hayo kwa mkopo kupewa sharti la msingi la kufanya kazi katika hospitali za umma kwa miaka isiyopungua mitatu.
Hiyo yote ikiwa ni njia ya kutatua changamoto ya watumishi wa afya katika hospitali za Umma kwani imeonekana kuwa wanafunzi wengi wa kada hiyo humaliza vyuo na kukimbilia kufanya kazi katika hospitali za binafsi au nje ya nchi na kuacha hoapitali hizo zikielemewa na idadi kubwa ya wagonjwa.
Mhe. Makonda alikaririwa akisema kuwa,” wanafunzi wanaosoma sekta ya afya kwa mikopo wanatumia bajeti kubwa ya Serikali na hizo zote zikiwa ni fedha za kodi za wananchi lakini mwisho wa siku wanaondoka bila kuwatumikia wananchi hao waliojitolea fedha zao kuhakikisha wanapata elimu”.
Aidha, Mhe Makonda aliupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kutenga eneo kwa ajili ya viwanda vya dawa na vifaa tiba pamoja na eneo litakalotumika kujenga kituo kikubwa cha utafiti wa masuala ya sayansi na liahidahidi kusaidiana nao kwa hali na mali katika kuhakikisha ujenzi wa chuo hicho unakamilika.
Njia nyingine ya kuhakikisha kuna kuwa na watumishi wa kutosha katika hospitali hiyo inayotarajiwa kuwa na watumishi 1300 ni kuhamisha watumishi kutoka katika hospitali mbalimbali nchini ambapo kwa kuanzia watumishi 928 wa awali wameshahamishiwa Hospitalini hapo.
Katika mkakati wa kuhakikisha wanaongeza idadi ya watumishi ili kuijengea uwezo na ufanisi hospitali hiyo serikali imetoa kibali cha kuajiri watumishi 50 katika mwaka wa fedha wa 2016-17  na wataendelea kuajiri kadiri bajeti itakavyoruhusu.
Kwa upande mwingine, Serikali imeamua kuweka historia nyingine ya kujenga kituo cha utafiti, mafunzo na tiba za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kitakachojengwa ndani ya eneo hilo la Mloganzila ambapo ujenzi huo unategemewa kuanza mnamo mwezi Mei mwaka 2017.
Mbali na kuongeza watumishi wa afya wenye weledi na kupunguza adha ya foleni katika hospitali zingine, nchi yetu pia itanufaika kwa kuwa na kituo hicho cha utafiti ambacho kitakuwa kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Ujenzi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania pamoja na Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ambapo kwa awamu ya kwanza ya mradi Serikali imetoa jumla ya shilingi 7,055,000 na ADB imetoa mkopo wa jumla ya shilingi 9,500,000.
 
Pia, ili kuhakikisha nchi yetu inapunguza gharama za wananchi kwenda kutibiwa nchi za nje, Serikali itachagua jumla ya wataalam 24 kutoka kada mbalimbali za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu kwa ajili ya kupewa mafunzo ya kina kuhusu magonjwa hayo katika hospitali za nje na ndani ya nchi ili waweze kubobea katika kutibu magonjwa hayo hivyo kupelekea wagonjwa kutibiwa hapa hapa nchini.
Kaimu Makamo Mkuu wa chuo hicho, Lyamula anaendelea kusema kuwa baada ya ujenzi huo kukamilika, uongozi wa chuo unajitahidi kwa hali na mali kutafuta mikopo na misaada mbalimbali nje na ndani ya nchi ili kuweza kuendeleza eneo lililobakia kwa ajili ya ujenzi wa chuo ambao ndio litakua chimbuko la wataalamu wa afya wenye utaalamu wa kutosha.
Aidha, alifafanua kuwa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 510,696,243 zinaendelea kutafutwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za waalimu, madarasa, maktaba, majengo ya utawala, mabweni ya wanafunzi, kumbi za mikutano pamoja na maabara.
Mkatati wa uboreshaji wa huduma za afya nchini hauishii tu kwenye kujenga hospitali mpya na za kisasa bali pia kuboresha maslahi ya wafanyakazi ili waendane na umuhimu wa kazi wanayoifanya kwaajili ya maendeleo ya nchi yetu.
Kwakuwa suala la afya ni suala mtambuka ambalo wadau wengi wa maendeleo wanatakiwa kushiriki ni vyema hata sekta binafsi ikaiunga mkono serikali kwa kupeleka huduma za afya kwenye maeneo ambayo hazipatikani ili kuweza kusaidiana na Serikali katika kufanikisha adhma ya kuwa na huduma bora za afya kwa wananchi hasa katika maeneo ya vijijini.

No comments:

Post a Comment