Tuesday, 17 January 2017

Rais wa Ufaransa asema Ulaya haihitaji ushauri wa Trump

Serikali ya uhamiaji iliwaruhusu wahamiaji kuingia nchini humo 2015
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amepuuzilia mbali hatua ya Rais mteule wa Marekani Donald Trump kukosoa sera ya Ujerumani kuhusu wahamiaji barani Ulaya.
Bw Hollande alisema hatua hiyo ya Bw Trump si ya busara.
"[Ulaya] haihitaji ushauri kutoka nje, kuambiwa inafaa kufanya nini," Bw Hollande alisema.
Bw Trump alikuwa amesema Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alifanya "kosa kubwa" kwa kuwaruhusu wahamiaji kuingia nchini mwake kwa wingi.
Bi Merkel kwa upande wake, akijibu tamko hilo la Trump, alisema bara Ulaya linafaa kuachwa lijifanyie maamuzi.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry pia alishutumu tamko hilo la Bw Trump.
"Nilifikiri, kusema kweli, kwamba haikufaa kwa rais mteule wa Marekani kuingilia siasa za mataifa mengine kwa njia ya moja kwa moja," Bw Kerry aliambia CNN.
"Atahitajika kuzungumzia hilo. Kuanzia Ijumaa (siku ya kuapishwa kwa Trump kuwa rais) ambapo atakuwa anawajibikia uhusiano huo."
Bw Trump pia amezua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa nchi wanachama wa muungano wa kujihami wa mataifa ya Magharibi (Nato) kwa kusema kwamba muungano huo umepitwa na wakati.
Aidha, ametishia kampuni za kuunda magari za Ujerumani kwamba ataziwekea kodi ya juu iwapo zitahamishia shughuli zake za uzalishaji Mexico.
'Kutangaza vita'
Akihojiwa na magazeti ya Uingereza na Ujerumani, Bw Trump alisema Umoja wa Ulaya (EU) umekuwa "kimsingi chombo cha Ujerumani".
Kuhusu kuingia kwa wahamiaji Ujerumani mwaka 2015, alisema: "Nafikiri alifanya kosa kubwa sana kwa kuwapokea wahamiaji hawa wote haramu..."


 Balozi wa Marekani nchini Ufaransa anayeondoka Jane Hartley akituzwa na Bw Hollande
Bw Merkel amesema EU inafaa kuruhusiwa kuendesha shughuli zake bila kuingiliwa
Bw Hollande, akizungumza mjini Paris, alisema EU iko tayari kuendeleza ushirikiano na Marekano lakini ushirikiano huo utaongozwa na "maslahi na maadili".
Alisema hayo alipokuwa anamtuza balozi wa Marekani nchini Ufaransa anayeondoka Jane Hartley, na kumpa medali ya heshima.



Mwanasiasa mwingine wa chama cha Kisosholisti, waziri mkuu wa zamani wa Bw Hollande, Manuel Valls, amesema tamko la Trump ni sawa na "kutangaza vita dhidi ya Ulaya".
Bw Valls anaonekana kuwa nyuma ya wapinzani wake katika uungwaji mkono kwenye kinyang'anyiro cha urais, uchaguzi mkuu unapotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.

No comments:

Post a Comment