
Aliyekuwa askofu mkuu wa kanisa katoliki mjini Jerusalem ambaye
alipatikana na hatia ya kuwapelekea silaha wapiganaji wa Palestina
amefariki akiwa na umri wa miaka 94.
Hilarion Capucci alihudumia kifungo cha miaka 12 jela nchini Israel
kabla ya Vatican kuingilia kati na kusaidia kumwachilia huru.
Alikuwa na historia ya uanaharakati unaohusishwa na mgogoro unaondelea mashariki ya kati.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas alituma risala za rambi rambi akimtaja kuwa alikuwa mpiganiaji wa uhuru.
Vatican ilithibitisha kifo chake siku ya Jumatatu ,lakini haikusema kiini cha kifo hicho ama hata kutoa maelezo.
Capucci alizaliwa katika mji wa pili kwa ukubwa nchini Syria Allepo mwaka 1922.
Alitawazwa kuwa kasisi wa kanisa la Allepo mwaka 1947 kabla ya kuteuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jerusalem.
Mwaka 1974, alikuwa akisafiri kutoka Beirut kuelekea Jerusalem ndani ya
gari lililokuwa na nambari za mwanadiplomasia wakati liliposimamishwa na
vikosi vya usalama vya Israel.
Ndani yake kulikuwa na bunduki nne aina ya Kalashnikov, bunduki nyengine
mbili aina ya pistol , silaha na maguruneti yalionuia kupewa wanachama
wa PLO.
Capucci alisisitiza kuwa ailazimishwa kusafirisha silaha hizo ,lakini
mahakama ya Israel ilimpata na hatia ya kusafirisha silaha na kumuhukumu
miaka 12 jela.
Aliachiliwa huru mwaka 1977 baada ya ombi la papa John Paul wa sita.
Capucci alisalia katika vyombo vya habari baada ya kuachiliwa kwake ,
akijaribu kuwa mpatanishi wa raia wa Marekani waliotekwa nchini Iran.
Ijapokuwa aliwakera baadhi ya mateka wa Marekani na matamshi yake wakati
alipowatembelea ili kuangalia hali yao 1980, alihusika pakubwa katika
usafirishaji wa miili minane ya wanahewa wa Marekani waliofariki katika
jaribio la kuwaokoa wenzao.
Mwaka 1990, alisafiri hadi nchini Iraq chini ya uongozi wa Saddam
Hussein ili kusaidia kuachiliwa huru kwa raia 68 wa Itali waliozuiliwa
kuondoka nchini humo kufuatia uvamizi wa Kuwait.
Miaka 10 baadaye Capucci aliongoza ujumbe wa viongozi wa dini na
wataalam nchini Iraq kwa umoja dhidi ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa.
Mwaka 2010, alikuwa ndani ya meli ya Mavi Marmara wakati meli hiyo ya
Uturuki ilioposimamishwa na makamanda wa Israel, iliposhiriki katika
usafirishaji wa misaada ili kujaribu kukiuka kizuizi cha Ukanda wa Gaza.
Wanaharakati 10 wa Uturuki , mmoja wao akiwa raia wa Marekani mwenye
uraia wa mataifa mawili ,waliuawa na makumi kujeruhiwa wakati ghasia
zilipozuka baada ya makamanda hao kuingia katika meli hiyo,wakishuka
kutoka kamba za helikopta.
Capucchi anasema kuwa uvamizi huo haukukubalika.
No comments:
Post a Comment