Tuesday 9 June 2015

Waziri Wasira azuru kaburi la hayati Karume, ashiriki dua.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira (wa pili kulia), akishiriki dua kwenye kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume mjini Zanzibar kabla ya kuanza ziara ya kutafuta wadhamini kwa ajili ya kuomba kuwania Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira, ametembelea na kushiriki dua kwenye kaburi la Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Abeid Amani Karume.
 
 Wasira aliingia visiwani Zanzibar juzi asubuhi ikiwa ni siku moja baada kuwasili kwa Waziri Mkuu wa zamani na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa.
 
 Wote wawili walionekana kwenye ofisi tofauti za CCM wakidhaminiwa na taarifa za uhakika zinaeleza kuwa hawakupata fursa ya kukutana.
 
 Lowassa alielekea kisiwani Pemba jana ambapo kwa upande wake, Wasira atakuwa huko leo.
 
 Alipofika Zanzibar, Wasira alikwenda Makao Makuu ya CCM, Kisiwandui na kuzungumza na Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Zanzibar), Vuai Ali Vuai na kufanya dua kwenye kaburi la  Rais wa Kwanza wa Zanzibar, hayati Karume.
 
 Akiwa mkoa wa Mjini, Wasira ambaye pia ni Mbunge wa Bunda, alisema akifanikiwa kuwania Urais na kushinda, atatetea Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
 
 Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini, Borafia Juma Silima, alisema hatua ya kujitokeza kwa wanachama wengi wanaoutaka Urais kupitia CCM, ni moja ya vielelezo vya kukua kwa demokrasia ndani ya chama hicho.
 
 Wilaya Mjini katika Mkoa wa Mjini palipofanyika udhamini kwa Wasira, ndipo penye Ikulu ya Rais, hospitali ya rufaa, Makao Makuu ya Polisi na hospitali ya wagonjwa wa akili.
 
 “Hiki ndicho chama chenye demokrasia pamoja na wingi wa wagombea, kila anayetaka atapita hapa ama kwa wenzetu wengine ili kudhihirisha kwamba hiki si chama cha mtu mmoja,” alisema.
 
 Aliongeza: “Naamini hiki kingine ni cha ufalme, mpaka aliyepo afe ndiyo arithi mwingine, sasa demokrasia imetanuka, wenye nia waje mjini hapa kudhaminiwa.” 
 
 Kwa upande wake, Wasira alisema Zanzibar inahitaji maendeleo, ustawi wa jamii na zaidi ya yote kulinda Muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
 
 Alisema akifanikiwa kupitishwa na CCM na kuchaguliwa kuwa Rais, ataifanya Tanzania isiruhusu Zanzibar kurudi kwenye utumwa na wanaodhani wanaishi kwa matumaini ya kurudi kwa hali hiyo (utumwa), itakuwa ni ndoto.
 
 “Nikiwa kiongozi, nchi itakuwa katika mikono salama ambayo ufisadi si sehemu yake,” alisema.

No comments:

Post a Comment