Thursday 18 June 2015

DK. Bilal ashauri urushaji wa matangazo ya runinga.

Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal.
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal (pichani), ametoa wito kwa Taasisi za Elimu na Afya kutumia mabadiliko ya urushaji matangazo ya televisheni kwa mfumo wa digitali kwa kutoa elimu kwa njia ya runinga ili kurahisisha utoaji masomo ya Sayansi na Historia kwa vijana.
 
Wito huo aliutoa jana katika sherehe ya ukomo wa urushaji matangazo ya televisheni kwa mfumo wa analojia jijini Dar es Salaam na kuwahusisha wadau mbalimbali.
 
Dk. Bilal alisema taasisi zinazohusika zinapaswa kusimamia kwa ukamilifu maudhui yanayowafikia wananchi ili yatumike kwa maendeleo na kuhakikisha kuwa channel za televisheni hazitoi mafundisho yasiyofaa kwa vijana  na  kuathiri  Taifa  la kesho.
 
“Tuna changamoto kubwa ya kutengeneza maudhui ya ndani ili tutangaze utamaduni wetu ndani na nje ya nchi kutokana na mfumo wa sasa wa digitali kujaa maudhui mengi kutoka nje,” alisema.
 
 Aidha, alizishauri taasisi zinazohusika zikishirikiana na wadau wote kutafuta mbinu bora na kutumia fursa ya mfumo wa digitali kutengeneza maudhui yatakayotangaza nchi, utamaduni, kukuza utalii nchini na kuimarisha amani, utulivu na uzalendo.
 
Aliipongeza Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa usimamizi na maelekezo sahihi waliyoyatoa wakati wote wa kipindi cha mabadiliko hayo na kuvishukuru vituo vyote vya televisheni ambavyo vilitoa ushirikiano mzuri na kuwezesha mabadiliko hayo 

No comments:

Post a Comment