Thursday 18 June 2015

Jaji Mkuu mstaafu ajitosa urais CCM

  Ajinadi kwa sifa 6, Dk. Shein kuchukua fomu urais Z'bar leo.
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani.
"Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu... Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza..."
 
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan, ametangaza nia ya kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku akieleza kuwa licha ya kuwapo kwa utitiri wa wagombea urais, hakuna Mtanzania yeyote anayeweza kumnyooshea kidole akimtuhumu kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa.
 
Jaji Ramadhan ambaye ni kada wa 36 kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa na chama chake kuwania kiti hicho, alisema hakuna mgombea anayemtisha kati ya wote waliomtangulia, kwa kuwa hakuna mwanajeshi anayeogopa.
 
Jaji Ramadhani alikuwa akizungumza na waandishi wa habari jana katika Makao Makuu ya CCM Mjini Dodoma, muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kuwania nafasi hiyo.
 
“Sina doa katika serikali au utumishi wangu; kwa kweli hakuna Mtanzania anayeweza kuninyooshea kidole kwa kupokea au kuhusika na vitendo vya rushwa. Kizuri chajiuza, kibaya chajitembeza. Mimi ni mwanajeshi, nimestaafu nikiwa Brigedia Jenerali Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Sijui kama kuna mwanajeshi anayeogopa na hakuna mgombea ninayemuogopa; nikiogopa ina maana mimi si mwanajeshi,” alisema na kuongeza: 
“Nina uzoefu wa kutosha, nina uwezo wa kuwatumikia Watanzania twende huko tunakotaka na kuinua uchumi wetu. 
 
Nimejipima na nimeona nina uwezo wa kugombea urais kwa sababu nakidhi vigezo vyote vinavyotakiwa kisiasa na kiuongozi; kilichonisukuma kutangaza nia ya kugombea ni uwezo wangu, sijashinikizwa na mtu yeyote,” alisema Jaji Ramadhani.
 
KUJIUNGA NA CCM
Kuhusu utata alijiunga lini na CCCM, wakati amekuwa mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 33, Jaji Ramadhani alisema:
“Nilijiunga na CCM mwaka 1969 nikiwa mwanafunzi wa mwaka wa tatu Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na niliendelea na uanachama wangu hadi 1992 kipindi mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa na kusababisha mabadiliko ya Katiba ambayo yaliweka masharti kwa mtumishi wa umma kutokuwa mwanachama.”
 
Jaji Ramadhani alisema baada ya mabadiliko hayo, uanachama wake ndani ya CCM ulisimama hadi mwaka 2010 alipostaafu nafasi ya Jaji Mkuu wa Tanzania na kulazimika kurejesha uanachama wake mwaka 2011 kwa ajili ya kuendelea na masuala ya siasa.
“Nilirudia uanachama wangu wa CCM mwaka 2011, baada ya kustaafu wadhifa niliokuwa nao kama Jaji Mkuu”.
 
RUSHWA
Kuhusu rushwa, alisema ni tatizo kubwa nchini. “Tatizo la rushwa katika serikali na nchi yetu ni kubwa, nataka nilimalize kama chama changu kitaniteua na kushinda nafasi hiyo…wakati nilipokuwa Jaji Mkuu, nilipambana nalo katika mahakama zetu,” alisema na kuongeza:
 
"Nawahakikishia Watanzania nikiwa Rais, ukila rushwa Kilimanjaro, hutahamishiwa Mtwara maana hata waliopo Mtwara ni Watanzania, hawataki mla rushwa.”
 
KATIBA MPYA
Alipoulizwa msimamo wake kuhusu mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya, Jaji Ramadhani alisema: “Kwa nafasi yangu niliyokuwa nayo kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kazi yetu ilikwishamalizika, baada ya kumkabidhi Rais Jakaya Kikwete, Rasimu ya Pili ya Katiba pale kwenye ukumbi wa Karimjee na Bunge Maalum la Katiba limemaliza kazi yake, hatua iliyobaki ni wananchi kuamua katika Kura ya Maoni. Na ndiyo itakayoamua hatma ya Katiba Mpya na si Rais.”
 
ASUBIRI ILANI
Alisema kwa sasa hawezi kuainisha vipaumbele vyake lakini iwapo atateuliwa kugombea urais, kazi yake kubwa itakuwa ni kutekeleza sera na siasa za CCM ambayo itakuwa imeainishwa ndani ya Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015.
 
ALIKOTOKEA
Jaji Augustino Ramadhani, alizaliwa Desemba 28, 1945 mjini Unguja, Zanzibar akiwa mtoto wa pili kati ya wanane waliozaliwa kwa wazazi wake. Baba yake ni Mathew Douglas Ramadhan, mkazi wa Zanzibar aliyefariki dunia mwaka 1962.
 
Alipata elimu ya msingi wilayani Mpwapwa, Dodoma katika Shule ya Msingi Mpwapwa, kati ya mwaka 1952 -1953 na baadaye alihamia mkoani Tabora na kusoma darasa la tatu na la nne katika Shule ya Msingi Town School mwaka 1954 – 1956. Mwaka 1957 – 1958, alisoma darasa la sita na la saba katika Shule ya Msingi Kazel Hill (sasa Shule ya Msingi  Itetemia), kabla ya kurudi Mpwapwa ambako alihitimu darasa la nane mwaka 1959.
 
Elimu yake ya sekondari aliipata katika Shule ya Sekondari ya Wavulana Tabora, kati ya mwaka 1960 hadi 1965.  Baada ya kumaliza elimu ya sekondari alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria kati ya mwaka 1966 hadi mwaka 1970.
 
Baada ya kuhitimu masomo ya Chuo Kikuu alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria na aliajiriwa na JWTZ kufanya kazi za uanasheria.
 
Mwaka 1971, alitunikiwa cheo cha Luteni akiwa kambi ya Mgulani jijini Dar es Salaam na miaka sita baadaye akahamishiwa Brigedi ya Faru mkoani Tabora wakati huo akiwa na cheo cha Meja.
 
Baadaye, Rais wa Zanzibar wakati huo, Aboud Jumbe Mwinyi, alimwomba na kumwondoa jeshini Jaji Ramadhani na kumteua kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) mwaka 1978.
 
Oktoba 1978, aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar. Mabadiliko mengine yalitokea Machi, 1979 na kurudishwa jeshini, ambako hakukaa muda mrefu; akahamishiwa vitani Uganda kuendesha Mahakama za Kijeshi (akiwa na cheo cha Luteni Kanali).
 
Baada ya vita, alirejea Zanzibar na kurudishwa kwenye utumishi wa kiraia ambako Januari 1980, aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar.
 
Miaka tisa baadaye, aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania.
 
Alidumu katika Ujaji wa Mahakama ya Rufaa kwa miaka minne hadi alipoteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) mwaka 1993. 
 
Alikaa Nec hadi Oktoba 2002 alipohamishiwa Zanzibar kufanya kazi kama Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) hadi Oktoba 2007. Mwaka 2007 aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania hadi alipostaafu mwaka 2010.
 
Jaji Ramadhani kwa sasa ni Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu yenye makao yake jijini Arusha.
 
SHEIN KUCHUKUA FOMU LEO
Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, leo anatarajia kuchukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuwania tena nafasi ya urais wa Zanzibar.
 
Dk. Shein atachukua fomu hizo katika ofisi kuu ya CCM Kisiwandui.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, Itikadi na Uenezi Zanzibar, Waride Bakari Jabu, Dk. Shein atakabidhiwa fomu hiyo na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai.
 
Waride alisema baada ya kukabidhiwa fomu hiyo, Dk. Shein atazungumza na viongozi wa CCM wakiwamo wa wilaya na mikoa ya Unguja.
 
Wengine ni wazee wa CCM na waasisi wa mikoa mitatu ya Unguja na Pemba.
 
Dk. Shein anakuwa mgombea wa kwanza wa CCM kuchukua fomu kuwania nafasi ya urais wa Zanzibar. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, hadi sasa hakuna jina la mwanachama wa CCM aliyetangaza nia ya kutaka kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi Zanzibar.
 
Mwishoni mwa wiki, wenyeviti wa CCM wa mikoa sita kichama, walitoa tamko la kumuomba Dk. Shein kuchukua fomu kuwania nafasi hiyo kutokana na uwezo wake wa kuisimamia na kutekeleza ilani ya chama hicho kwa mafanikio makubwa.
 
Dk. Shein ataungana na mgombea wa nafasi ya urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye ameshachukua fomu ya kuwania nafasi hiyo baada ya kuidhinishwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa la chama chake.
 
Imeandikwa na Godfrey Mushi,  Editha Majura, Dodoma na Rahma Suleiman, Zanzibar

No comments:

Post a Comment