Saturday 20 June 2015

Baraza la Madiwani Tabora laridhia kukamwatwa Elibariki Kingu



BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Mkoani Tabora limeridhia agizo lililotolewa na Mkuu wa kitengo cha upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Tabora la kumkamata aliyekuwa mkuu wa wilaya ya Igunga,Elibariki Kingu anayetuhumiwa kutafuna shilingi milioni 95 zilizotolewa na Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo kwa vijana mwaka 2013.


makubaliano hayo yalifikiwa katika kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika juzi kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo,kikiwa na agenda moja tu ya kutaka kufahamu endapo Elibariki Kingu alishazirejesha fedha za vijana hao.

Katika kikao hicho cha baraza,diwani wa kata ya Isakamaliwa kwa tiketi ya CCM,Dotto Kwilasa katika swali lake la msingi alimtaka Mkuu wa polisi awaeleze kuhusu watu wanaotuhumiwa kula fedha za vijana zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha vijana ni kwa nini hadi siku hiyo walikuwa hawajakamatwa,wakati suala hilo wao kama madiwani walilikabaidhi jeshi la polisi.

“Mh,Mwenyekiti leo tunataka mkuu wa polisi atuambie kuhusu hawa watu waliokula fedha za vijana zilizotolewa na serikali kwa ajili ya kuwawezesha vijana ni kwanini hadi leo hawajakamatwa wakati sisi kama madiwani suala hili tuliwakabidhi jeshi la polisi”alihoji diwani huyo kwa mshangao mkubwa wa kutotekelezwa agizo hilo.

Akijibu swali la diwani huyo,Kaimu Mkuu wa polisi wilaya ya Igunga,Joeli Marunga alisema tayari ofisi ya Afisa Upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Tabora (RCO)imeagiza kwamba aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Igunga,Elibariki Kingu,Mwenyekiti wa SACCOS ya vijana pamoja na wenzake wanatakiwa kukamatwa na kufikishwa Mahakamani.

Aidha kaimu kamanda huyo wa jeshi la polisi,Marunga aliendelea kuliambia baraza la madiwani hao kwamba kwa mujibu na taratibu,lengo la kukamtwa watuhumiwa hao ni kuhakikisha fedha wanazotuhumiwa kuzitafuna wanazirudisha.

Kwa mujibu wa msemaji huyo,vilevile katika makosa ya kughushi na kuiba watuhumiwa wake huwa wanakamatwa,kushtakiwa na hatimaye kufilisiwa mali walizonazo na kurudishiwa wahusika wa fedha hizo.

Hata hivyo kamanda Marunga aliwaomba madiwani hao kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili watuhumiwa wote waweze kukamatwa kwa haraka kwa vile wao madiwani wanawatambua vizuri.

Kadhalika pamoja na maamuzi hayo,hata hivyo baadhi ya madiwani,Anjela Milemba na Henry Athumani walisema kwamba muda wao umekaribia kwisha,hivyo wanataka kabla hawajaondoka madarakani washtakiwa wawe wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani.
Naye Mwanasheria wa Halmashauri hiyo,Gwandumi Mwambage alisema kesi ya jinai itaendelea kushughulikiwa na jeshi la polisi na kwamba wao kama Halmashauri watashughulikia kesi ya madai namba 8 waliyofungua Mahakama ya wilaya Igunga,dhidi ya kikundi cha vijana Saccos.

Kufuatia tuhuma hizo,nilimtafuta aliyekuwa Mkuu wa wilaya ya Igunga,Elibariki Kingu ili kujua juu ya tuhuma zinazomkabili lakini licha ya kupigiwa simu na kutumiwa ujumbe mfupi wa maandishi,lakini hakuwa tayari kupokea simu yake wala kujibu ujumbe mfupi wa maandishi.

Akiahirisha kikao cha baraza la madiwani,Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Igunga,Emmanuel Samson aliliomba jeshi la polisi wilayani Igunga kutekeleza agizo la Afisa wa upelelezi wa kitengo cha makosa ya jinai (RCO) pamoja na baraza la madiwani ili kikao kijacho cha mwisho wa mwezi,waweze kupeleka majibu juu ya kukamatwa kwa watuhumiwa.

No comments:

Post a Comment