Monday 1 June 2015

Mwigulu Nchemba: Nitawavusha Watanzania


Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba akizungumza na wananchi kwenye Ukumbi wa Chuo cha Mipango Dodoma alipotangaza nia ya kugombea urais kupitia CCM jana.
Dodoma/Dar. Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba ametangaza nia yake ya kugombea urais kupitia CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba akieleza jinsi atakavyoivusha Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati utakaopatikana kwa kutoa haki kwa watu wote.
Akitangaza nia hiyo jana kwenye Ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango Dodoma, Nchemba alisema: “Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Nitawavusha wanaCCM wenzangu pamoja na Watanzania kwa ujumla… wakati ni sasa tunataka Taifa letu lifike kuwa nchi yenye uchumi wa kati,” alisema Nchemba na kuongeza:
“Ninachoomba kutoka kwenu, mniamini na mniunge mkono katika hili… nitawavusha. Lakini tukumbuke kwamba kila mmoja lazima atimize wajibu wake katika utendaji kazi ili tufikie huko tunapotaka kufikia.”
Nchemba aliyekuwa ameongozana na mkewe, Neema na watoto wake watatu, Isaack, Grecious na Joshua pamoja na ndugu jamaa na marafiki, alisisitiza kuwa ili kufikia malengo hayo, lazima nchi iwe na mfumo wa uwajibikaji utakaowezesha kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza Pato la Taifa.
Huku akitumia kauli mbiu ya ‘Mabadiliko ni Matendo, Wakati ni Sasa’, ambayo ataitumia katika safari yake ya kuelekea Ikulu, Nchemba aliyetumia dakika 115, kuanzia saa 10.10 jioni hadi saa 11.25 jioni, alisema atapambana na tabia za watu kufanya kazi kwa mazoea, rushwa, ufisadi na kwamba Serikali ya Awamu ya Tano atakayoiongoza endapo atachaguliwa, itakuwa ya uadilifu na uaminifu.
Alisema iwapo atachaguliwa, ataifanya nchi kuwa ya kipato cha kati sambamba na watu wake, kujenga Taifa linalojitegemea kibajeti na kuwajengea uwezo wananchi kumiliki uchumi wao wenyewe.
Huku akieleza jinsi atakavyomaliza kilio cha ukosefu wa ajira, wanafunzi, wakulima, wafanyakazi, wafanyabiashara na watu wa kada mbalimbali nchini, Nchemba alianza hotuba yake kwa kuwashukia baadhi ya watu wenye dhana potofu juu ya mtu anayestahili kuwa rais wa nchi.
“Nimeamua kutangazia nia hapa Dodoma kwa sababu ndipo makao makuu ya nchi na kama nikiwa rais nitaapishiwa hapa. Pia sikutaka kutangazia nia nyumbani Iramba ili kuondokana na umimi,” alisema na kushangiliwa na mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo.
Awajibu wanaomponda
“Uzoefu ni mazoea ya starehe. Mtu aliyekaa katika uongozi ni mtu aliyesahau shida za Watanzania.
Jambo la kwanza na la msingi ni kuitambua ajenda ya Watanzania, Watanzania watamuunga mkono kiongozi kwa kuitambua ajenda yake,” alisema.
Alisema wakati akijitathimini kutangaza nia ya kugombea alikuwa akifahamu ajenda ya Watanzania, huku akisisitiza kuwa umaskini hakuusoma katika vitabu, bali amekulia katika maisha ya kimaskini.“Ukizungumzia ukosefu wa ajira na dawa hospitali hilo sijalisoma vitabuni, ukizungumzia ajira kwa vijana na watu wote hilo jambo sijalisoma vitabuni.”
Alisema katika pitapita zake, amesikia habari za mtu anayefaa kuwa rais zikihusishwa na umri na uzoefu, “Ujana na uzee haviwezi kuwa sifa ya kuiongoza nchi. Kukaa serikalini muda mrefu haiwezi kuwa sifa ya kutosha kuliongoza Taifa hili, unaweza ukakaa sana serikalini lakini ukasababisha hasara kubwa. Hata kuishi ni hivyohivyo, kinachoangaliwa si kuishi miaka mingi, bali ni kipi ulichokifanya. Leo hii marehemu (Edward) Sokoine hakumbukwi kwa sababu alikaa sana serikalini, anakumbukwa kwa matendo yake kwa kipindi kifupi alichokaa serikalini.”
Huku akishangiliwa alisema, “Kiongozi akipatikana kwa mazoea atafanya kazi kwa mazoea. Vita ya kwanza tunayotaka kuikomesha katika nchi yetu ni kufanya kazi wa mazoea. Tunahitaji mambo matatu; mabadiliko, mbinu za kufanya mabadiliko na utayari wa kufanya mabadiliko.”
Kuhusu umri alisema: “Wengine wanaongelea umri wamesahau kuwa Katiba inasema umri wa kugombea ni miaka 40, hata vitabu vitukufu vimeandika kwamba umri wa miaka 40 ni sahihi mtu kupewa utume na unabii, Mussa alipofikisha miaka 40 aliaminiwa kwenda kuwakomboa ndugu zake.”
Alisema hata Mwalimu Julius Nyerere alikuwa rais akiwa na miaka 40, tena akitoka kufundisha sekondari.
“Watu wanataka kuwatoa Watanzania katika ajenda kwa kuzungumzia vitu vyepesi. Eti wanasema ukimaliza kuwa rais wakati bado kijana utafanya nini. Nifanye nini tena wakati nitakuwa nimeshamaliza kazi. Najipambanua kwa ajenda yangu na wale watakaoniangalia wataangalia ajenda yangu,” alisema.
Mipango yake
“Kwa miaka 50 tumekuwa tegemezi, sasa imetosha tunakwenda kujitegemea. Kujitegemea ni kila mmoja kulipa kodi anayostahili,” alisema.
Alisema wakati wa watu wachache kubeba mzigo wa kodi umefikia mwisho na kwamba kila mtu anayestahili kulipa atailipa, awe mdogo au mkubwa.
“Tunakwenda kuachana na utaratibu wa kukimbizana na wauza vitumbua kuwadai kodi. Kujitegemea ni nidhamu ya matumizi na sasa tunakwenda kuziba mianya ya rushwa,” alisema.
Alisema ili uchumi umilikiwe na Watanzania wenyewe, lazima njia za kuwapatia watu kipato ziboreshwe kwa sababu uchumi wa nchi unakua lakini wananchi bado wanalia umaskini.
“Njia ya kuwatoa hapo walipo ni kuongeza thamani ya mazao na kazi wanazozifanya kwa sababu asilimia 70 ya Watanzania ni wakulima. Lazima wakulima watafutiwe pembejeo na masoko. Tunatakiwa kutumia sekta binafsi ili kuwa na viwanda vingi nchini,” alisema na kutoa mfano:“Pamba ya Tanzania inaweza kutumika kutengeneza sare za shule, za jeshi na viatu kutoka katika viwanda vilivyopo nchini. Tuna wanafunzi zaidi ya milioni nane na kila mwaka wanaandikishwa shule, kwa nini tulilie soko la nje halafu sare zao tunanunua nje.”
Kuhusu mafuta, Nchemba alisema kilimo cha alizeti kikiboreshwa kitazalisha ajira nyingi na hilo linaweza kufanyika pia katika sukari, kahawa, chai na korosho.
“Awamu ya tano, nchi itaingia katika uchumi wa viwanda na vijana watafanya kazi kwa kupokezana,” alisema.
Mwigulu aligusia suala la Watanzania kutozwa kodi zisizokuwa na kichwa wala miguu na zisizoendana na uzalishaji wa biashara husika, huku akitolea mfano mama ntilie na wamachinga.
“Wakubwa wakitaka kuwekeza wanapewa likizo ya miaka 10 ya kulipa kodi lakini anayefungua saluni anatozwa kodi wakati akiwa anapaka rangi jengo hata biashara hajaanza,” alisema na kushangiliwa.
Rushwa
Akizungumzia rushwa alisema: “Rushwa hupofusha macho ya wenye akili na kurejesha nyuma maendeleo na hupindisha ukweli na kuwanyima haki maskini.”
Alisema awamu zote nne za Serikali zimejitahidi kupambana na rushwa, ila awamu ya tano itakuja na njia tofauti kwamba atakayethibitika kupokea au kutoa rushwa atachukuliwa hatua haraka ili iwe fundisho.
“Sasa hivi mtu akikamatwa na rushwa kesi zimekuwa na mlolongo mrefu. Tutabadilisha Sheria namba 11 ya Kupambana na Rushwa ili kuipa meno Takukuru iweze kushughulika na suala hili na atakayebainika atafilisiwa, kufukuzwa kazi na kufungwa,” alisema.
Alisisitiza: “Habari ya mtu kula rushwa ya fedha nyingi na kuondolewa katika cheo chake ni sawa na kumpa likizo, ni sawa na kumfanyia ‘send off’ kwa fedha za walipakodi.”
Kufanya kazi kwa mazoea
Akizungumzia suala la kufanya kazi kwa mazoea alisema: “Serikali ya awamu ya tano itaondokana na ukiritimba unaoondoa ufanisi. Hakutakuwa na ucheleweshaji wa kutoka kwa ajira kwa kisingizio cha kibali. Nchi hii ina upungufu wa wafanyakazi kila wizara na taasisi.Lazima ufanyike utaratibu wa kujua idadi ya vijana wasio na kazi ili waweze kupatiwa nafasi. Inakuwaje mtu anastaafu halafu unasema hakuna wa kuziba pengo lake!”
Alisema anazungumzia uchumi kwa sababu ameusomea na kusisitiza, “Kuna matatizo kwenye mgawanyo wa keki ya Taifa. Leo hii watu wakipewa dhamana ya kusimamia shirika la umma wanachokifanya ni kutafuna fedha za walipakodi. Jambo hili haliwezekani maana kuna wajawazito wanalala chini.”
“Haiwezekani sungura akawa mdogo kwa baadhi ya Watanzania na sungura huyohuyo akawa mkubwa kama tembo kwa baadhi ya Watanzania. Haiwezekani shirika la umma wakalipana posho za juu huku watoto wa maskini wanakosa mikopo. Nitakomesha rushwa kwa kuzingatia masilahi ya wafanyakazi,” alisema.
Alisema ni wakati wa Tanzania kuwa nchi ya viwanda na katika kuthibitisha hilo, hayatafanyika makosa tena katika uwekezaji wa gesi kwa kuweka wazi mikataba na fedha zitakazotokana na mauzo ya gesi lazima zihifadhiwe katika akaunti za benki za ndani ya nchi.
Kuhusu elimu na afya, alisema sasa umefikia mwisho wa wananchi kununua dawa.
“Kila anayeugua anaambiwa akanunue dawa lakini kila mwaka mnasikia Serikali inadaiwa fedha za dawa. Katika hili tutadhibiti kila kitu ikiwamo wale wanaoiba dawa na tukimbaini tutamnyang’anya leseni yake na atakwenda jela,” alisema.
Kuhusu elimu alisema: “Miaka mitatu ijayo tutakuwa na wanafunzi wengi na tutahitaji zaidi ya Sh700 bilioni kwa ajili ya mikopo, kazi iliyopo mbele yetu ni kuweka chanzo maalumu kwa ajili ya elimu ya juu ili mtoto yoyote mwenye sifa asikose nafasi ya kwenda chuo kikuu kwa sababu tu ya kukosa mkopo.”
Pia aligusia suala la kuimarisha ulinzi na usalama na Muungano ambao alisisitiza kuwa ni lazima ulindwe na kuifanya Zanzibar kuwa na uchumi wa viwanda.
Katika hotuba yake, Mwigulu alisema ili kumaliza migogoro ya wakulima na wafugaji ni lazima kugawa ardhi kwa kila upande.
Kura za wanaCCM
Katika hotuba yake Nchemba aliwaangukia wanachama wa CCM akisisitiza kuwa amejitathimini vya kutosha na anaweza kukiongoza vyema chama hicho na Watanzania wote.
“Ahadi yangu kubwa kwenu ni kwamba nitawavusha. Kabla ya kufika kwa Watanzania nitaomba ridhaa ya wanaCCM. Ninakijua chama hiki na ahadi yangu kwenu nitawaunganisha wanaCCM na Watanzania wengine,” alisema.“Tunakwenda kukomesha kufanya kazi kwa mazoea na kusimamia rasilimali na kuweka usawa, haya ndiyo tunasema ni mabadiliko kwa vitendo na wakati wa kufanya hayo ni sasa. Taasisi zote za usimamizi nafasi zake zitapatikana kwa ushindani,” alisema.
“Anayeanzisha kibanda cha kibiashara lazima aandaliwe mazingira ya biashara yake. Tunawahamisha wamachinga kwa kigezo cha kusafisha jiji utadhani wao ni uchafu. Ukiwaondoa wakati walikuwa wakifanya kazi halali watarudi na kufanya kazi zisizo halali,” alisema.
Alisema anaomba ridhaa kwa wanaCCM ili akafanye kazi mapinduzi katika Taifa na kuleta haki, heshima na upendo katika eneo lililotawala na chuki.
“Naomba mambo matatu, kwanza mniamini, mniunge mkono na jambo la tatu nitawavusha. Kwenye vita ya umaskini mimi ni mtu sahihi, wakati sahihi na muda sahihi ni sasa,” alisema.
Ajibu maswali
Alipoulizwa kuhusu hotuba yake ya kama haimhatarishii mbio zake za kuelekea Ikulu, Nchemba alisema hana shaka na chama chake wala Watanzania na ndiyo maana amesema atawavusha.
Kuhusu atakavyoshughulikia rushwa kubwa kama za EPA, Meremeta na Escrow ambazo watuhumiwa wake wameonekana wakitanua na fedha hizo, alisema sifa moja ya mtu anayeweza kupambana na rushwa ni yeye kutokuwa mla rushwa.
Alisema iwapo atapata ridhaa ya Watanzania, rushwa litakuwa ni janga na hivyo litashughulikiwa kama tatizo maalumu... “Adhabu kali itatolewa ili mtu asirudie tena kufanya hivyo.”
Alisema siyo rushwa kubwa tu, bali nyingine zinazotokana na ununuzi wa umma ambao watu wamekuwa wakipandisha juu bei ya bidhaa... “Hatutakuwa na uvumilivu katika mazingira haya.”
Ilivyokuwa
Kuanzia saa 7.00 lango la ukumbi wa Mwalimu Nyerere katika Chuo cha Mipango na Maendeleo ulikuwa wazi na idadi kubwa ya watu walianza kuingia wengi wakiwa vijana kutoka mikoa ya Dodoma na Singida huku kukiwa na idadi kubwa ya viongozi wa dini.
Wabunge waliohudhuria ni Ally Keissy, Omary Badwel, Modestus Kilufi, Martha Mlata, Asumpta Mshama na baadhi ya wabunge kutoka Zanzibar.Mbali na madiwani, makatibu na wenyeviti wa CCM kata na mitaa kwa Manispaa ya Dodoma, Katibu wa CCM Mkoa Albert Mgumba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Anton Kanyama.
Wengi wa vijana waliovaa fulana za rangi za Bendera ya Taifa huku wengi wakivaa skafu kama anavyovaa wakati wote Nchemba.
Baba mzazi wa Mwigulu, Mzee Madelu Nchemba na mama yake, Asha waliongoza wanafamilia ya Naibu Waziri huyo kutoka Kijiji cha Makunda Wilaya ya Iramba mkoani Singida.
Nje ya ukumbi, mabango yaliyojaa picha zake yalipambwa zikiwa na maandishi, “Mabadiliko ni kwa vitendo, wakati ni sasa,” ambayo wengi walikuwa wakipiga picha hapo. Mengine ni kupanga ni kuchagua na kutenda ni kwa vitendo, wakati ni sasa.
Mabango yaliyobebwa na vijana yalikuwa na ujumbe mbalimbali ukisomeka, Mwigulu mkombozi wa Watanzania 2015, Mwigulu ni Sokoine aliye hai 2015 njia ni nyeupe.

No comments:

Post a Comment