Friday 5 June 2015

Makinda kuongoza mazishi ya Mwaiposa Dar, Marehemu Kamishna Malisa kuzikwa Kilimanjaro.

Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Anne Makinda.

Spika wa Bunge la Jamhuri la Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, ataongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Mbunge wa Ukonga, (CCM) Dar es Salaam, Eugen Mwaiposa (55).
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dodoma na Idara ya habari, elimu kwa umma na uhusiano wa Kimataifa-ofisi ya bunge, imeeleza kuwa Spika Makinda ataongoza mazishi ya mbunge huyo ambayo yatafanyika  Juni 6, mwaka huu. nyumbani kwake Kipunguni, Dar es Salaam baada ya watoto marehemu walioko nje ya nchi kuwasili.
 
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mwili wa marehemu umeshawasili Dar es Salaam na kupokelewa na waombolezaji wakiongozwa na Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, na kuhifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Jeshi ya Lugalo.
 
Wakati huo huo, Mkuu wa Jeshi la Magereza mkoani Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi Mwanadamizi, Venant Kayombo,  leo anatarajiwa kuongoza mamia ya waombolezaji katika mazishi ya aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, Onel Malisa.
 
Mtoto wa marehemu, Emmanuel Malisa, alikuwa Kamishna kuanzia mwaka 1996 hadi 2002.
 
Marehemu alizaliwa mwaka  1944, alipata elimu ya msingi, sekondari, Chuo Kikuu.
 
Alijiunga na Jeshi la Magereza mwaka 1964 na kuhitimu mafunzo ya awali ya uaskari yaliyofanyika Chuo cha Magereza-Ukonga, Dar es Salaam kuanzia Januari –Julai mwaka huo, 1964.
 

No comments:

Post a Comment