Saturday 20 December 2014

Unamkumbuka Nyamayao?






Dar es Salaam. Kama ulibahatika kutazama tamthilia miaka ya 1990 - 2003, basi jina la Nyamayao na Kibakuli siyo geni masikioni mwako na hata sura zao.
Watoto hawa wawili walikuwa wanaunda familia ya Mhogo Mchungu. Ni familia iliyokuwa na visa vingi hasa baada ya Mhogo Mchungu kutaka kumuoza Nyamayao ilhali alikuwa bado kigori. Hadithi hii ninaikumbuka pindi ninapokutana ana kwa ana na Nyamayao ambaye kwa sasa ni mama wa familia.
Kibakuli amebadilika hivi sasa si mnene kama alivyokuwa mdogo, lakini kwa Happyness Wenslaus ‘Nyamayao’ bado ana umbo na kimo kilekile, ni kati ya waigizaji wa kike ambao wanajitunza kwani hajabadilika licha ya kupata umaarufu akiwa binti mdogo.
Mwananchi lilifanya mahojiano na mwigizaji huyu ambaye alizungumza mengi, kuhusu anachokifanya kwa hivi sasa, kilichomfanya aachane na uigizaji, kwanini ameamua kuirudia upya sanaa na hata ndoto za maisha yake ya baadaye.
Kwa miaka 11 umekuwa nyuma ya kamera na hujatokea tena katika tamthilia wala filamu kulikoni?
Nimekaa muda mrefu kimya kwa sababu tamthilia yangu ya mwisho nimeigiza mwaka 2003 baada ya hapo nikamaliza elimu ya sekondari na hapo nikajiunga na Chuo cha Uandishi wa Habari DSJ, nilipomaliza chuo nikawa na mambo mbalimbali ya kwangu binafsi.
Ina maana sanaa ndiyo umeipa kisogo?
Ndiyo maana unaniona niko na wasanii wenzangu ina maana kwamba ninarudi tena kwa kasi. Kwa sasa hivi ninafanya tamthilia, tumejikusanya wasanii ambao tulikuwa tunafanya kazi zamani kipindi cha nyuma, na tukaunda kikundi kipya ambacho kinaitwa ‘Kaone Sanaa Group’. Na tumeanza kufanya tamthilia ambayo Mungu akipenda mwakani mwanzoni itaanza kuonekana runingani.
Miezi michache nyuma iliwahi kuelezwa kwamba unaigiza filamu imeishia wapi na ni filamu gani?
Nimefanya filamu za watu kama mbili hivi, japokuwa hazijaingia sokoni nimefanya ya kwangu mwenyewe moja na sasa hivi nimejikita rasmi katika tamthiliya. Kuna filamu niliyoifanya mwenyewe imetoka miezi mitatu iliyopita, hizi za watu wengine hazijatoka ‘Malipo’ na ‘Prosoner’.
Kwa faida ya wasomaji nini kilikuweka mbali na sanaa ya uigizaji?
Mambo ya maisha na majukumu yangeniweka mbali na familia, wakati mwingine ukishaingia katika familia kuna watoto na nini kuna vitu lazima uhakikishe umeviweka sawa. Kwa upande wangu si kwamba nilikuwa nimeacha ila kuna mambo yalinilazimu niache kwanza.

 




No comments:

Post a Comment