Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda cha sabuni cha
KEDS wilayani Kibaha, Bw. Jack Feni (Kushoto kwake) kuhushu mitambo
ya kiwanda hicho hicho wakati alipokitembela September 19, 2017.
Kulia kwake ni. Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mahandisi Evarest Ndikilo na
kulia ni Mbunge wa Kibaha Mjini, Silyvestry Koka.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amewataka viongozi wa mkoa wa Pwani waboreshe miundombinu ya maeneo
waliyoyatenga kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili waweze kuwavutia
wawekezaji wa nje na ndani.
Ametoa agizo hilo leo (Jumanne,
Septemba 19, 2017) wakati akizungumza na kwa nyakati tofauti na
wafanyakazi wa kiwanda cha kutengeneza sabuni ya unga cha Keds kilichopo
Kibaha na kiwanda cha kutengeneza vigae cha Twyford kilichopo Chalinze.
Waziri Mkuu amesema ameridhishwa
na kasi ya maendeleo ya ujenzi wa viwanda mkoani Pwani na amewaagiza
viongozi wahakikishe maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji yanakuwa
na miundombinu muhimu kama maji, umeme na barabara.
“Nimefarijika kuona miradi hii
mikubwa ya ujenzi wa viwanda ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika,
nawashukuru kwa kuunga mkono mkakati wa Rais Dkt. John Magufuli wa
kukuza uchumi kupitia sekta ya viwanda.”
Amesema mbali na viwanda hivyo
kutoa ajira nyingi kwa Watanzania, pia vitakapoanza uzalishaji
vitawawezesha wananchi kupata bidhaa mbalimbali kama vigae kwa bei nafuu
kwa kuwa vitakuwa vinazalishwa nchini.
Pia Waziri Mkuu amewataka wananchi
wanaofanyakazi kwenye viwanda hivyo wawe mabalozi wazuri wa Taifa kwa
kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu mkubwa ili kuwathibitishia
wawekezaji kwamba wao wanauwezo mkubwa wa kufanya kazi na hakuna haja ya
kutafuta wafanyakazi kutoka nje ya nchi.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa
viwanda hivyo Bw. Jack Feng amesema ujenzi wa huo umekamilika kwa
asilimia 90 na sasa wako katika hatua za mwisho ikiwa ni pamoja na
ufungaji wa mitambo na vinatarajiwa kuanza uzalishaji Oktoba mwaka huu.
Amesema vigae watavyovizalisha
wanatarajia kuviuza kwa gharama nafuu kwa sababu asilimia 95 ya
malighafi inapatikana ndani ya nchi. Pia ameahidi kutoa ajira nyingi kwa
wananchi waishio kwenye maeneo yanayozunguka viwanda hivyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa
Pwani, Mhandisi Evarest Ndikilo amemuomba Waziri Mkuu awasaidie
upatikanaji wa nishati ya umeme ya kutosha kuweza kuendesha viwanda
katika mkoa huo.
Mhandisi Ndikilo amesema mahitaji
waliyonayo ya nishati ya umeme ni megawati 92, ambapo kwa sasa
wanasambaziwa megawati 40, hivyo ameomba suala hilo lipatiwe ufumbuzi wa
haraka ili lisije kuathiri uzalishaji.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, SEPTEMBA 19, 2017.
No comments:
Post a Comment