Kaimu Meneja wa Mawasiliano toka
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Semu Mwakyanjala akifafanua jambo
kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akielezea matumizi
sahihi na salama ya mitandao ya kompyuta na intaneti mapema hii leo
jijini Dar es Salaam, kulia ni Afisa Habari wa Idara ya habari (MAELEZO)
Bi. Fatma Salum.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
Na Fatma Salum – MAELEZO
Serikali kupitia Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa rai kwa Watanzania kuacha kutumia
vibaya mitandao ya simu na intaneti badala yake waitumie kwa ajili ya
kurahisisha harakati zao za kujiletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa leo na Kaimu
Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo Bw. Semu Mwakyanjala wakati
akizungumza kwenye mkutano na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam.
Mwakyanjala alisema kuwa licha ya
teknolojia ya mawasiliano kukua na kuleta faida kwenye jamii yetu, bado
kuna changamoto nyingi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha
anatumia vizuri mitandao hiyo kwa faida yake na taifa kwa ujumla.
“Kutokana na mabadiliko ya kila
siku ya teknolojia hasa kwenye sekta ya mawasiliano imesababisha baadhi
ya watu kutumia vibaya teknolojia hiyo kupitia mitandao ya kompyuta na
intaneti kufanya uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo wizi, utapeli,
ulaghai na uchochezi,” alieleza Mwakyanjala.
Pia alibainisha kuwa wapo baadhi
ya watu wasiokuwa wazalendo ambao hutumia mitandao hiyo kusambaza
taarifa zenye maudhui ya chuki au uchochezi na kuongeza kuwa Serikali
haitasita kuwachukulia hatua kali za kisheria .
Mwakyanjala alisema kuwa Serikali
inaendelea na jitihada za kusimamia usalama mitandaoni kupitia Kitengo
cha Dharura cha Kuitikia Matukio ya Usalama Kwenye Mitandao (TZ-CERT)
ambacho kinafanya kazi ya kuratibu matukio ya usalama katika mitandao ya
kompyuta na intaneti kwa kushirikiana na vyombo vingine husika vya
kikanda na kimataifa.
Akieleza mambo muhimu ya
kuzingatia kwa watumiaji wa huduma za mitandao, aliwataka watumiaji hao
kuwa makini na taarifa zao binafsi wanazoweka kwenye mitandao ya kijamii
pamoja na kutumia program za kujikinga na virusi hatarishi katika
kompyuta na simu zao.
“Ni jukumu la kila mmoja
kuhakikisha kwamba anajilinda na uhalifu wa mitandaoni na kuepuka
kumtajia mtu mwingine taarifa zake binafsi kama vile neno la siri
(password) kwani kufanya hivyo kunawarahisishia watu wenye nia mbaya
kufanya uhalifu,” alisisitiza Mwakyanjala.
Aidha alibainisha kuwa matumizi ya
mtandao yamepanuka sana nchini ambapo kwa sasa Tanzania kuna watumiaji
wa mtandao wanaokadiriwa kufikia milioni 18 ukilinganisha na mwaka 2011
ambapo kulikuwa na watumiaji milioni 5 tu.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) ilianzishwa mwaka 2003 kwa sheria na. 12 kwa lengo la kusimamia
na kudhibiti mawasiliano ya kielektroniki na huduma za posta.
No comments:
Post a Comment