Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwasalimia wananchi wa Chemba mkoani Dodoma wakati alipolazimika
kusimama baada ya kuona umati mkubwa wa wananchi hao waliokuwa
wakimsubiri alipokuwa akisafiri kwa Barbara kwenda Arusha akitoka
Dodoma Septemba 20, 2017.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akiwasalimia wananchi wa kijiji cha Kalema wilayani Chemba wakati
alipolazimika kusimama baada ya kuona umati mkubwa wa wananchi hao
waliokuwa wakimsubiri alipokuwa akisafiri kwa Barbara kwenda Arusha
akitoka Dodoma Septemba 20, 2017.
Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi
na salama pamoja na huduma ya umeme katika maeneo mbalimbali nchini
zikiwemo wilaya za Chemba na Kondoa mkoani Dodoma.
Amesema Serikali kupitia Kampeni
ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi
katika maeneo yote nchini watapata huduma ya maji safi na salama katika
umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.
Waziri Mkuu aliyasema hayo jana
(Jumatano, Septemba 20, 2017) alipozungumza kwa nyakati tofauti na
wananchi wa wilaya ya Chemba na Kondoa waliomsimamisha katika maeneo ya
Chemba, Kalema, Bicha na Bereko akiwa njianu kuelekea mkoani Arusha kwa
shughuli za kikazi.
Alisema kwa sasa Serikali
imeendelea na uchumbaji wa visima virefu, vifupi pamoja na kuweka
mtandao wa mabomba ya kusamba maji katika maeneo mbalimbali nchini
yakiwemo na ya wilaya hizo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hiyo
karibu na makazi yao.
Pia Waziri Mkuu alisema wananchi
wanatakiwa wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za
kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani
ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu
aliwaagiza watendaji wawachukulie hatua watu wote watakaokutwa
wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na
uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha
ukame.
Akizungumzia kuhusu upatikanaji wa
nishati ya umeme, Waziri Mkuu alisema hakuna kijiji nchini
kitakachoachwa bila ya kuunganishiwa huduma hiyo katika awamu ya tatu ya
Mradi wa Nishati Vijijini (REA).
Ameagiza wakandarasi wamalize
maeneo yaliyosalia katika REA awamu ya pili ndipo waendelee na awamu ya
tatu. Alisema Serikali imetenga sh. trilioni moja kwa ajili ya kusambaza
umeme katika vijiji 8,000 ambavyo bado havijaunganishiwa nishati hiyo.
“Rais wetu Dkt. John Magufuli
anajali sana wananchi wake, hivyo ametenga fedha nyingi
zitakazotosheleza kusambaza umeme katika vijiji vyote vikiwemo na vya
wilaya za Chemba na Kondoa. Gharama za kuunganishiwa umeme huo ni sh.
27,000 tu.”
Pia Waziri Mkuu alisema
mwananchi hawatowajibika tena katika kulipia nguzo wala fomu za maombi
ya kuunganishiwa umeme, kwa sababu tayari gharama hizo zimeshabebwa na
Serikali.
Waziri Mkuu aliongeza kwamba
lengo la Serikali ni kufikisha umeme kwenye vijiji vyote Tanzania na kwa
vile ambavyo viko kwenye maeneo yaliyo mbali na gridi vitafungiwa sola,
jambo ambalo litafungua fursa za ajira na kukuza uchumi.
Awali mbunge wa Chemba, Bw. Juma
Nkamia, Mbunge wa Kondoa Mjini Bw. Edwin Sanda na Naibu Waziri wa Fedha
na Mipango Dkt Ashatu Kijaji ambaye ni Mbunge wa Kondoa Vijijini
waliomba Serikali iwasaidie katika kutatua kero ya maji na umeme.
Walisema katika maeneo mbalimbali
ya majimbo yao wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya
umeme pamoja na maji safi na salama hivyo kusababisha wananchi kushindwa
kushiriki vema kwenye shughuli za kimaendeleo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, SEPTEMBA 21, 2017.
No comments:
Post a Comment